NA SAKINA MASOUD, DODOMA
MWENYEKITI wa CCM mkoa wa Dodoma, Alhaj Adam Kimbisa, amewataka wanachama wapya 200 waliojiunga na CCM katika Kata ya Chifutuka wilayani Bahi kuwa waaminifu na waadilifu bila ya kuhangaika na vyama vinavyoundwa kiukoo.
Alhaj Kimbisa alitoa rai hiyo juzi wakati akikabidhi kadi katika muendelezo wa ziara yake ya kuangalia utekelezaji wa Ilani, kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa mwenyekiti na kuangalia uhai wa Chama katika Mkoa wa Dodoma.
Alisema CCM ndio chama pekee ambacho kipo kwa ajili ya kila mtu, tofauti na vyama vingine ambavyo ukiangalia hata majina yao ni yale yale ya kutoka kule kule.
Wanachama wenzangu mliokula kiapo leo (juzi) msibabaike na vyama vingine, CCM imewazaa, imewalea na mnazeeka mkiwa nayo, msiwe kama baadhi ya watu ambao sio waaminifu wanaoonekana asubuhi wakiwa CCM, mchana CHADEMA na usiku anakuwa CUF,”alisema.
Pia, aliwataka wananchi wa kata hiyo kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi unaokuja na kusisitiza kuchagua mtu aliye tayari kuwatumikia wakati wote wa uongozi wake na asiye tayari kutoa au kupokea rushwa.
Ndugu zangu uchaguzi unakuja na mna nafasi ya kugombea nafasi yoyote mnayoona inafaa kwako, lakini wajibu wenu mkubwa ni kuangalia aina ya kiongozi mnaemchagua nyinyi wenyewe ili kesho na keshokutwa msilalamike maana mtakuwa mmemchagua wenyewe,”alisema Kimbisa.
Kimbisa aliwaahidi kuwa kama mkoa hawatakata jina la mgombea yoyote aliyependekezwa na wananchi na kuwasisitiza kuhakikisha kura zote wanapeleka CCM.
Katika ziara yake kwenye kata hiyo aliahidi kupeleka ‘solar’ katika Shule ya Sekondari ya Magaga ili wanafunzi waweze kusoma vizuri.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru