- Ni waliotafuna bil. 28/- za ushirika
- Adaiwa kuwabeba wasiadhibiwe
- Wakulima wamshitaki kwa Kinana
- Mkuu wa mkoa, mbunge wamjia juu
NA MOHAMMED ISSA, SIKONGE
WAKULIMA wa Tumbaku katika wilaya za Sikonge na Uyui mkoani Tabora, wamemshukia Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza kwa kushindwa kuwachukulia hatua vigogo wa vyama vya ushirika waliotafuna sh. bilioni 28 za wakulima.
Wamesema pamoja na Mhandisi Chiza kupatiwa ripoti ya ukaguzi wa wizi wa mabilioni hayo ya wakulima, ameshindwa kuwafukuza kazi na kuwafikisha mahakamani.
Mbali na hilo, wamelalamikia gharama za usafirishaji wa pembejeo kutoka Dar es Salaam mpaka Tabora, ambapo wamesema mfuko mmoja wa pembejeo unasafirishwa kwa sh. 12,000 tofauti na wa saruji ambao unasafirishwa kwa sh. 2,000.
Wamebainisha kuwa, mbinu hizo za usafirishaji wa pembejeo zinafanywa na maofisa wa vyama vya ushirika kutoka wizarani.
Wamesema ujenzi wa maghala ya kuhifadhia Tumbaku, uliogharimu mabilioni ya fedha, hauna kiwango na yameanguka huku gharama hizo zikibebwa na wakulima, jambo linalozidi kuwatia umasikini.
Walisema gharama za ujenzi wa maghala hayo iliongezwa kwa asilimia 125 na waliofanya hivyo walikuwa na nia ya kujipatia ulaji.
Licha ya malalamiko hayo, wakulima hao walisema wanatakiwa kulipa kwa dola za Marekani wakati wao wanalipwa kwa shilingi ya Tanzania tena kwa mkopo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima hao walisema ripoti ya ukaguzi iliyofanywa na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, imebainisha viongozi wa vyama vya ushirika ni wezi, lakini hadi sasa wanaendelea kukingiwa kifua na Mhandisi Chiza.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru