Tuesday, 13 May 2014

Aliyeua wazazi wake mbaroni


NA WILIUM PAUL, HAI
POLISI mkoani Kilimanjaro, wanamshikilia Yusufu  Njau (32), mkazi wa Kijiji cha Roo, wilayani Hai, kwa tuhuma za kuwaua wazazi wake kikatili kwa kuwakatakata mapanga.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Robert Boaz, alithibitisha jana kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
“Mtuhumiwa amekamatwa jana, saa 12.00 asubuhi, nyumbani kwa kaka yake, Alifa Shaibu,” alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo, Mei 9, mwaka huu, saa 12 jioni, katika Kijiji cha Roo, ambapo aliwaua baba yake mzazi na mama yake kwa kuwakatakata kwa mapanga sehemu za kichwani na kisha kuchoma moto nyumba waliyokuwa wanaishi.
Njau, anadaiwa kuwaua baba yake Shahibu Hassan (60) na mama yake Minae Mohamed (57), ambao walizikwa Mei 10, mwaka huu, katika makaburi ya familia kijijini hapo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Roo, Alfani Swai, alisema mtuhumiwa huyo alitoka alikokuwa amejificha jana asubuhi baada ya kushikwa na njaa kali.
Aliamua kwenda nyumbani kwa kaka yake aitwae Alifa Shaibu, aishie karibu na Shule ya Sekondari ya Roo, kwa nia ya kuomba chai.
Swai, alisema baada ya mtuhumiwa huyo kufika nyumbani hapo, ndipo kaka yake huyo aliamua kupiga simu kwa mwenyekiti kumuarifu kuwepo kwa mtuhumiwa huyo ndipo alipowasili na kukuta umati wa watu.
“Wakazi walitaka kumpiga, lakini niliwasihi wasijichukulie sheria mkononi ambapo mjomba wake alimchukua na kumpeleka katika kituo cha Polisi Bomang’ombe ili hatua za kisheria zifuate,” alisema.
Baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, wananchi walisema kwa sasa wataishi kwa amani kutokana na kuwa na mashaka na mtuhumiwa huyo anayedaiwa kuwa alikuwa akiwasumbua sana kijiji hapo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru