Na Mwandishi wetu
HOFU ya kupoteza soko kwa kampuni za kigeni zinazozalisha umeme dhidi ya kampuni ya kitanzania imetajwa kuwa chanzo cha vita dhidi ya kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Chanzo cha uhakika kutoka Wizara ya Nishati na Madini, kimetoa taarifa hiyo kwa gazeti hili jana kuwa kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, kampuni za kigeni zimekuwa zikipata faida kubwa kwa kuzalisha umeme na kuuza kwa bei ya juu nchini.
Kampuni ya IPTL ambayo inamilikiwa na kampuni ya kizalendo, Pan African Power Solutions Tanzania Limited (PAP), iliishtua dunia mwishoni mwa mwaka jana pale ilipotangaza dhamira ya kushusha bei kutoka senti za Marekani 26 na 30 ya sasa mpaka senti sita na nane kwa kila uniti, pale itakapobadilisha mitambo yake kuweza kutumia gesi badala ya mafuta.
Kwa sasa, kampuni nyingine katika soko zinatoza kati ya senti za Marekani 38 na 60 kwa kila uniti.
“Watanzania wasidanganywe na taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa IPTL ilinunuliwa na PAP bila kufuata sheria.
“Kuna kampeni ya kupakana matope kwa tamaa ya kuzalisha umeme kwa Watanzania kutokana na biashara hii kuwa na faida kubwa,” kilisema chanzo hicho.Kampuni ya PAP katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam, ilisema imeshtushwa na baadhi ya wawekezaji katika sekta hiyo na wanasiasa, kuanzisha vita dhidi yao baada ya kutangaza kupunguza gharama za umeme.
Uongozi wa kampuni hiyo ulisema Watanzania watafurahia gharama hizo za chini baada ya utekelezaji wa mkakati wao wa utanuzi na ubadilishaji wa mfumo wa mitambo yao ambao utaongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme kutoka megawati 100 za sasa mpaka megawati 500.
Katibu na mshauri wa masuala ya sheria wa IPTL/PAP, Joseph Makandege, alisema kampuni hiyo imekuwa ikikumbana na changamoto ambazo zinajaribu kuzorotesha jitihada za uongozi mpya za kuleta mabadiliko ambayo yatasababisha kampuni hiyo kuanza kuzalisha umeme wenye gharama nafuu kwa wananchi.
Taarifa hiyo ya Makandege, ilitolewa baada ya taarifa mbalimbali za vyombo vya habari kuishutumu kampuni hiyo zikidai inatoa hongo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, lengo likiwa kuwalinda dhidi ya tuhuma mbalimbali wanazo husishwa nazo.
“Uongozi wa PAP katu haujapendezwa na jitihada za kuiangusha kampuni badala ya kushirikiana katika kuhakikisha kuwa tunazalisha umeme ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa hili na walaji wote nchini.
“Tukiwa ni kampuni ya ufuaji umeme, tunaelewa faida za kiuchumi zitokanazo na umeme wa gharama nafuu kwa mteja mmoja mmoja na kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi nzima.Kwa sababu hiyo, ndiyo maana sasa tumeelekeza jitihada zetu katika kuona ni jinsi gani ya kuzaliza umeme wa gharama nafuu ambao utasaidia kuleta mabadiliko ya kiuchumi, pasipo kuingia katika malumbano ambayo yataturudisha nyuma na kushindwa kutekeleza lengo letu la kuwekeza vilivyo katika sekta hii muhimu,” ilisomeka taarifa hiyo.
Makandege, alisema kampuni yake imeamua kutafuta njia nzuri ya kuzalisha umeme wa gharama nafuu, ukilinganisha na wazalishaji wengine katika soko.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru