NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
SERIKALI imesema ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, Mahakama Kuu zote, Mahakama za Mikoa na Mahakama za wilaya nchini, zitakuwa zinatumia teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), katika ukusanyaji na utunzaji wa takwimu.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro, aliyasema hayo jana Bungeni, alipokuwa akiwasilisha Makadirio ya Matumizi ya Wizara yake, kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015.
Alisema kwa sasa Tanzania imejiimarisha katika matumizi ya TEHAMA katika mahakama zake kwa upatikanaji wa takwimu mbalimbali za kimahakama.
Dk. Asha Rose, Alisema mfumo huo kwa sasa umeanza kutumika Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu katika Divisheni ya Biashara, Kazi na Ardhi na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Dk. Asha Rose, alisema serikali imekamilisha upembuzi yakinifu kuhusu mradi wa ‘e- justice’ utakaorahisisha uendeshaji wa mashauri ya jinai.
Alisema mradi huo utaunganisha Mahakama, Magereza na Ofisi za mikoa za Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa njia ya mtandao, ambapo kwa sasa ripoti ya kazi hiyo imewasilishwa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango na Wizara ya Fedha, kwa hatua za uamuzi.
Alisema mpaka sasa masijala 68 za Mahakama za Mwanzo zimeboreshwa kwa kuwekewa mfumo wa kielektroniki za kutunza kumbukumbu za majarada.
Alisema mfumo huo umerahisisha upatikanaji wa taarifa za kimahakama na hivyo kuondoa mianya ya rushwa.
Akizungumzia mikakati ya wizara yake katika kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani, Waziri huyo alisema imeongeza kasi ya kusikiliza mashauri yaliyosajiliwa mahakamani.
Mkakati huo umeweka wastani wa idadi ya mashauri yatakayosikilizwa na kila ngazi ya mahakama kwa kila mwaka.
Kwa mujibu wa Dk. Asha Rose, katika Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, lengo ni kumaliza mashauri mapya ndani ya miezi 24, Mahakama ya Hakimu Mkazi katika muda usiozidi miezi 18 na Mahakama za Mwanzo kumaliza mashauri mapya ndani ya miezi 12.
Alisema mkakati huo umesaidia kupungua mashauri kwa kiasi kikubwa, ambapo hadi Desemba 2012, Mahakama ya Tanzania ilikuwa na mashauri 114,278 yaliyohusu madai, jinai na ardhi.
Alisema katika mwaka 2013, mahakama ilisajili mashauri mapya ya aina hiyo 168,068 na kufanya idadi ya mashauri yaliyokuwepo kufikia 282,346.
Thursday, 15 May 2014
Mahakama zote kutumia TEHAMA
07:46
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru