Tuesday, 13 May 2014

Mwigulu: Tutakufa na vigogo wakwepa kodi


“Hatuwezi kuwabana wauza vitumbua wakati kuna matajiri wanakula kuku kwa kuhujumu uchumi.
Na Latifa Ganzel, Morogoro
SERIKALI imetangaza vita na baadhi ya wafanyabiashara nchini wanaofanya hujuma kwa kukwepa kulipa kodi, huku wengine wakijificha kwenye mwamvuli wa taasisi za kidini na uzawa.
Pia, imewaonya watumishi wake ambao ni vinara wa kushirikiana na wafanyabiashara hao kukwepa kodi na kusababisha serikali kupoteza mapato, kuwa kamwe hawatapona.
Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema kuanzia sasa, serikali itapambana kufa kupona dhidi ya wafanyabiashara na mawakala wake wanaoshiriki kukwepa kodi.
Mwigulu, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyasema hayo jana kwenye ziara ya kukagua maendeleo na miradi ya maji wilayani Gairo, Morogoro.
“Tutakufa na wafanyabiashara hawa na tayari tumeingia rasmi kwenye mapambano. Kuna mawakala ambao ni watumishi wa serikali wanaoshirikiana na wafanyabiashara hawa, tunaomba wenye taarifa rasmi watupatie,” alisema Mwigulu na kuongeza: Hatuwezi kuwatoza kodi wauza vitumbua wakati kuna matajiri wakubwa wanakwepa kodi.”
Pia, alisema tayari serikali iko kwenye hatua za mwisho wa kuwasilisha bungeni sheria ya kufuta misamaha ya kodi kwa baadhi ya wafanyabiashara na taasisi ambazo hazistahili.
Huku akishangiliwa na umati wa watu, Mwigulu, alisema sheria mpya itakayowasilishwa bungeni, itatumika kuwabana kikamilifu wakwepa kodi wote.
“Kuna matajiri wakibanwa kulipa kodi wanaanza kuwatumia wananchi kama kivuli na kulalamika kuwa wanaonewa, wakati ni wahujumu uchumi wakubwa. Wanakwepa kodi kwa kigezo cha uzawa na kutokuwa na uwezo.
“Ukiweka kodi kwenye simu wanashindwa kulipa, lakini kila siku wanakatwa fdha kwa kuweka milio kwenye simu zao,” alisema.
Hivi karibuni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, aliwalipua baadhi ya wabunge kuwa wanatuhumiwa na baadhi ya wafanyabiashara nchini kukwamisha muswada wa sheria ya kufuta misamaha ya kodi.
Zitto, alisema tayari wafanyabiashara hao wameanza kuwatumia wabunge kama kinga ili kuhakikisha muswada huo unakwama waendelee kuihujumu serikali.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru