Tuesday 18 February 2014

Wasomi washauri serikali mbili

NA Khadija Mussa

WASOMI wamesema mfumo wa serikali tatu ni changamoto na mzigo mkubwa kwa Tanzania, hivyo ni vyema uliopo kwa sasa wa serikali mbili ukaendelea. 
Wameshauri kuwa mfumo wa serikali moja unaweza kuwa suluhisho na kuwaunganisha Watanzania, lakini kwa sasa utekelezaji wake ni mgumu.
Pia, wamesema ni vyema kukawekwa utaratibu maalumu wa kuwaenzi waasisi wa Muungano na kuendeleza misingi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mpango wa Utafiti wa Vyuo Vikuu Kusini Mashariki mwa Afrika (ESAURP), Profesa Ted Maliyamkono, alisema kero za wananchi haziwezi kutatuliwa kwa kuwa na serikali tatu.
Aliyasema hayo wakati wa mkutano wa kujadili Katiba Bora ya Tanzania uliojumuisha wasomi takribani 100 kutoka Angola, Botswana, Tanzania, Kenya, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Swazland, Uganda, Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini.
Uifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Alisema kwa mujibu wa utafiti walioufanya, serikali moja ndiyo itakayoweza kuwaunganisha wananchi na kutatua kero zinazowakabili.
“Tathmini inaelekea katika serikali moja, lakini kabla ya kufika huko inabidi tuendelee na iliyopo kwa sasa (serikali mbili), kwani hatuwezi kuwa na serikali tatu au nne,” alisema.
Mhadhiri wa Sheria za Katiba na Haki za Binadamu, Dk. Charles Kitima, alisema suala la kuwa na serikali tatu ni jibu la kukata tama.
Alishauri waasisi wa taifa waenziwe kwa kuwa na serikali moja.
Alisema ni lazima watu wahakikishe ndoto za waasisi wa taifa zilizoasisiwa mwaka 1964 za kuwa na serikali moja zinatimizwa, kwani waliona ni vyema waanze na mbili ili lengo la kuwa na serikali moja lije baadaye.
Dk. Kitima, alisema taifa imara linapaswa kuwaenzi waasisi wake, hivyo misingi iliyowekwa inatakiwa kuendelezwa na watu wasianze kuunda taifa, badala yake warudi katika misingi iliyowekwa wakati waasisi hao walipoamua kuungana.
Naye Profesa Peter Kagwanja ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Africa Policy kilichopo Nairobi, Kenya, alisema suala la serikali tatu ni changamoto na kushauri wananchi wakubaliane na mfumo wa sasa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru