Wednesday 19 February 2014

Chipaka: Ni serikali mbili

Na Peter Orwa, Dodoma

WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza msimamo wa muundo wa serikali mbili, Rais wa TADEA, John Chipaka, amesema ataunga mkono iwapo hoja ya chama hicho ya serikali moja haitakubalika.
Chipaka, mmoja wa magwiji wa harakati za siasa za vyama vingi nchini, alisema hayo wakati wajumbe wa vyama vya upinzani katika Bunge Maalumu la Katiba mjini hapa wakiweka mkakati wa kuungana kutetea hoja ya serikali tatu.
Akizungumza katika viwanja vya Bunge mjini hapa jana, Chipaka alisema hoja ya serikali tatu haikubaliki, kwa sababu zitakuwa mzigo kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Chipaka, hoja hiyo pia inapingana na waasisi wa taifa waliounda Muungano wa serikali mbili, wakilenga kuelekea serikali moja.

“Nakubaliana na wanaosema serikali tatu zitaongeza mzigo,” alisema na kuongeza kuwa, mizigo hiyo ni kuwa na marais wengi na jeshi zaidi ya moja. 
Habari zilizopatikana mjini hapa zinasema vyama vya upinzani vimekuwa vikikutana ndani ya majengo ya bunge vikipanga mikakati ya kushirikiana, ikiwemo kuhusu hoja ya Muungano.
Chipaka alikataa kushiriki vikao hivyo vinavyodaiwa kuratibiwa na CHADEMA chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Taarifa zinasema katika kikao cha juzi, washiriki walitofautiana huku wale wa vyama vidogo wakidai wamekuwa wakitengwa lakini linapotokea jambo kama hilo ndipo wanapoombwa ushirikiano. Katika hatua nyingine; CHADEMA imekuwa ikifanya ushawishi ikitaka kuungwa mkono kuhusu uraia wa serikali mbili.
Baadhi ya wabunge wa chama hicho wanadaiwa kupita kuwashawishi wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuwaunga mkono.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru