Thursday 13 February 2014

Dk. Bilal ahimiza usimamizi wa amani

NA JANE MIHANJI

VIONGOZI wa dini wametakiwa kuhubiri amani na kuwakemea bila woga wenye nia ya kuivuruga.
Wito huo ulitolewa juzi, jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, alipotembelea maonyesho ya picha za kazi zinazofanywa na Mtukufu Aga Khan.

Alisema nchi haiwezi kuendelea bila kuwepo amani. 
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal
"Hatuwezi kukaa, kusali makanisani, misikitini na katika nyumba zingine za ibada kama majumbani mwetu kumechafuka."
Dk. Bilal aliwasihi viongozi wa dini kuendelea kutoa mafunzo ya kazi za kijamii ili wananchi wajikite katika maendeleo na kujiinua kiuchumi.
Alisema wajibu wa viongozi wa dini hauishii katika elimu ya kiroho pekee, kwa kuwa waumini wanahitaji huduma zingine za kimwili na kiakili.
Makamu wa rais alipongeza juhudi zinafanywa na Jumuia ya Ismailia katika kuenzi na kuendeleza kazi ya kiongozi wao, Mtukufu Aga Khan,  kwa kuwasaidia wasiojiweza.
Alisema wana-jumuia ya Ismalia wamekuwa wakitoa huduma kadhaa, zikiwemo za elimu na kushiriki katika masuala ya uchumi na afya nchini.
"Huu ni mfano wa kuigwa katika biashara, faida wanayoipata ndiyo huwasaidia watu wengine, tunatakiwa kujifunza katika hili," alisema.

Viongozi mbalimbali, wakiwemo mawaziri wamekuwa wakitembelea maonyesho hayo, ambayo Rais mstaafu Benjamin Mkapa anatarajiwa kuyatembelea leo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru