Tuesday 18 February 2014

Mkutano biashara Manyara kuanza leo

Na Mwandishi wetu, Manyara

MKUTANO wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Manyara ambao ulikuwa unasubiriwa kwa muda mrefu tangu kufanyika kwa Kongamano kubwa la Uwekezaji mwaka jana, unafanyika leo chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa huo, Elaston Mbwilo.
Mbwilo aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa kwamba maandalizi yote ya mkutano huo muhimu yamekamilika na moja ya agenda kuu itakuwa matokeo ya kongamano la uwekezaji na utekelezaji wake.
“Wajumbe wote kutoka sekta za umma na ile binafsi wamethibitisha ushiriki wao hapo kesho (leo) na kila kuhusiana na mkutano wetu kipo safi,” alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Mbwilo alisema mkutano huo una maana kubwa sana ikizingatiwa kuwa mwaka jana uliandaa kongamano kubwa la uwekezaji ambalo lilivuta wawekezaji wengi wa ndani na wale wan je hivyo utatoa nafasi kubwa kwa wajumbe kujadili matokeo yake kwa kina.
“Wajumbe wa baraza watapata fursa ya kupitia utekelezaji wa mambo yote yaliyokubaliwa wakati wa kongamano ambalo lilihudhuriwa pia na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,” alisema.
Akifafanua zaidi umuhimu wa mkutano huo, Mbwilo alisema tangu kuanzishwa kwa baraza hilo la biashara mkoa, sekta za umma na binafsi zimekuwa zikifanya kazi kwa ukaribu mkubwa na hivyo kuibua fursa mbalimbali za kibiashara.
“Mkoa huu Manyara una utajiri mkubwa sana na sisi kama baraza la mkoa tunatumia mikutano kama huu kujadiliana kwa kina ni namna gani tunaweza kutumia fursa hizi kubadilisha maisha ya watu na kujenga kujenga uchumi imara.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Mhandisi Raymond Mbilinyi, ambaye anahudhuria mkutano huo, amelisifu baraza la Mkoa wa Manyara kwa kuandaa mkutano na kuiomba mikoa mingine kufanya hivyo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru