Friday 28 February 2014

CCM moto Kalenga


NA MWANDISHI WETU, KALENGA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), jana kilizindua kwa kishindo kampeni zake za ubunge katika Jimbo la Kalenda, Iringa,  kwa kumnadi mgombea wake, Godfrey Mgimwa, ambapo maelfu ya wananchi walihudhuria.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, akimnadi mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga, Godfrey Mgimwa, wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM, uliofanyika jana, uwanja wa Chuo cha Ifunda, Iringa . (Picha na Bashir Nkoromo). 

Katika uzinduzi huo ambao ulitawaliwa na shangwe, nderemo na vifijo huku wananchi wakieleza bayana kuwa watampigia kura Mgimwa siku ya upigaji kura kwa kuwa sera zake zimekuwa na matumiani makubwa.
Naibu Katibu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, aliwaeleza kamwe wasidanganywe na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, kwa kuwa ana mapepo.
Mwigulu ambaye alikonga nyoyo za wananchi wa Kalenga, alisema baada ya Dk. Slaa kuacha kumtumikia Mungu, kwa sasa mawazo na mtazamo wake vimejikita katika kusema uongo na uzushi licha ya kuwa mtu mzima.
Akizungumza katika kijiji cha Ifunda,  wakati akizindua kampeni hizo, alisema CCM imemsimamisha mgombea makini na kijana mwenye uwezo wa kuwaletea wananchi maendeleo.
“Kwa sasa Dk. Slaa ana miaka 70, lakini ana mchumba na kichwa chake kimekuwa kikisema mambo ya uongo na kuhamasisha maandamano,’’ alisema Mwigulu huku akishangiliwa.
Pia alisema iwapo atatakiwa kumtaja mtu mmoja kati ya ambao hawaheshimu basi atamtaja Dk. Slaa na hilo linatokana na tabia zake za kusema uongo kwenye majukwaa ya kisiasa.
Alisema kuhangaika huko kwa Dk. Slaa, kunatokana na kulipwa mamilioni ya shilingi ambazo CHADEMA wanapewa kama sehemu ya ruzuku hivyo, ni lazima apige domo.
Aliwaasa wananchi wa Kalenga kumchagua Mgimwa kwa kuwa CCM ndiyo yenye Ilani inayotekelezwa tofauti na wapinzani ambao kazi kubwa ni kuhamasisha vurugu.
“Tunahitaji maendeleo ya wananchi wa Kalenga. Tumchague Mgimwa na tuachane na hawa wapiga kelele wakiongozwa na babu (Dk. Slaa), ambaye anahangaika kutafuta kula yake,’’ alisema.
Alisema kuwa ilani ya inayotekelezwa sasa ni ya CCM na upinzani hauna wanachotekeleza na hata kusimamia mgombea wao ni ushamba wa siasa.
“Kinachoendelea sasa ni kutekeleza maendeleo kupitia Ilani ya CCM ambayo wanayoimiliki ni wa CCM,” alisema.
Alisema umefika wakati kwa wananchi kumtuma kijana wao Mgimwa ili akafanye kazi ya kuleta maendeleo yao na si kuchagua mbunge kwa sababu tu ya kuchagua.
Mwigulu aliwaomba, wananchi kuacha ushabiki katika mambo ya maendeleo, hivyo hawatakiwi kufanya kosa kwa kumchagua mtu ambaye anatoka nje ya CCM.
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Njombe, Pindi Chana, alisema wananchi wanahitaji maendeleo na si maandamano.
Alisema anashangazwa na CHADEMA kushindwa kutatua matatizo ya wananchi na badala yake wanazunguka hewani kwa helkopta wakati wananchi wako chini.
Akizungumza katika mkutano huo, Chifu wa Kabila la Wahehe, Abdul Mkwawa, alisema kuwa kamwe hawezi kuwa CHADEMA na wanaozusha kuwa amemkaribisha Dk. Slaa wanajisumbua.
Alisema kuwa yeye ni kada wa CCM na ataendelea hovyo na kwamba damu yake ni CCM.
“Siwezi kuwa CHADEMA, wamezusha hadi kwenye mitandao eti nimemkaribisha Dk. Slaa Kalenga na wanadai mimi ni CHADEMA. Si kweli kwanza huyo Dk. Slaa wa kazi gani huku kwetu,” alisema.
Nape acharuka, atoa
angalizo kwa Mangu
SIKU mbili baada ya kutangaza kujiunga na CCM, waliokuwa madiwani wawili wa CHADEMA katika Manispaa ya Shinyanga, wameanza kutishiwa maisha.
Hatua hiyo imetokana na kile kilichoelezwa hasira za baadhi ya viongozi kuchukizwa na uamuzi wa madiwani hao, Sebastian Peter (Ngokolo) na Zacharia Mfuko (Masekelo), ambao walijiuzulu nyadhifa hizo kutokana na chama hicho kukosa mwelekeo na dhamira ya dhati ya kuwatumikia watanzania.
Wakizungunza juzi wakati wakitambulishwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mahakama mjini Shinyanga, walisema wamekuwa wakipokea simu na kauli za vitisho kutokana kwa baadhi ya viongozi na wafuasi wa CHADEMA.
Walisema uamuzi wa kujiondoa CHADEMA na kujiunga na CCM umelenga kupata fursa ya kuwatumia wananchi na kamwe hawatakaa wajutie.
Kutokana na vitisho hivyo, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ambaye aliwatambulisha rasmi kwenye mkutano huo, amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Ernest Mangu, kuchukua hatua kwa wahusika wote.
Pia alisema vitisho wanavyopewa makada wake hao ni ishara kuwa CHADEMA kimezoea kutesa wanachama wanaokihama hivyo, hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kuwalinda.
Akizungumza kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na umati mkubwa, Nape alilitaka jeshi la polisi kuwapa ulinzi na kufuatilia viongozi wa chama hicho wanaowatishia maisha.
‘’Wametoka CHADEMA kwenye mavurugu wamerejea nyumbani kwa ajili ya kuungana na viongozi makini ndani ya CCM na serikali yake ili kuwatumikia watanzania. Sasa wameanza kutishiwa maisha, naomuomba IGP Mangu afanyie kazi taarifa hizo na kuwapa ulinzi hawa makada wetu. Hii ni tahadhari na kamwe hatukubali iwapo watadhurika kwa namna yoyote ile. Tutaanza na polisi kisha tutamaliza na waliowadhuru,’’ alisema Nape huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Alisema limekuwa jambo la kawaida kwa wanachama wa CHADEMA wanaopenda mabadiliko kuitwa majina ya wasaliti au wahaini pamoja na kuwasukia mizengwe kutokana na kutokuwepo kwa demokrasia.
Alisema kuna wanasiasa waliojaribu kutaka kufanya mabadiliko ya kuigeuza CHADEMA kutoka kuwa taasisi ya kifamilia na kuwa chama cha siasa, lakini wamekwama kutokana na mizengwe na wengine wamefukuzwa.
“Chama halisi na makini kwa maslahi ya watanzania ni CCM, ndio sababu hawa wenzetu wamerudi nyumbani. Milango iko wazi kwa wengine kurejea CCM kwa sababu wenzetu wana taasisi ya kifamilia si chama cha siasa,’’ alisema Nape.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru