Friday 28 February 2014

Kampuni za simu mtegoni

NA MOHAMMED ISSA
RAIS Jakaya Kikwete amezindua mtambo utakaodhibiti mapato ya kampuni za simu nchini hivyo kuiwezesha serikali kukusanya mapato yake kwa ufanisi.
Pia ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha wanadhibiti mawasiliano ya ndani na sehemu zingine za serikali.

RAIS Jakaya Kikwete

Amesema kuanzia sasa ni lazima kuwepo kwa sheria maalumu za mitandao zitakazowezesha nchi kuwa salama kupitia mitandao hiyo.
Rais Kikwete alisema hayo jana Dar es Salaam, alipozindua mtambo huo, ambao pia utahakiki mawasiliano ya simu za nje ya nchi.
 Alisema mtambo huo utaiwezesha serikali kupata mapato yake kwa uhalali na kwamba katika mwaka itakusanya wastani wa sh. bilioni 20.
“Kabla ya mtambo huu, kampuni za simu zilikuwa zinakadiria mapato na kuleta serikalini lakini sasa tutaweza kukusanya fedha nyingi zaidi. Mtambo huu utawezesha kufahamu kila kampuni inapiga simu ngapi na wanapata kiasi gani hivyo itakuwa rahisi kwa serikali nayo kupata mapato yake kwa utaratibu unaostahili,” alisema.
Alisema serikali imeamua kuwekeza kwenye sekta ya mawasiliano kwa sababu ni kichecheo muhimu cha uchumi wa nchi.
Rais Kikwete alisema kwenye sekta ya mawasiliano TCRA inafanya vizuri na kwamba serikali inaridhishwa na namna inavyofanya kazi zake.
“Kufanya kazi na watu kama ninyi inaleta raha sana, mko tofauti na wenzenu ambao unatoa maagizo wanasema tuko kwenye mchakato au tuko mbioni,” alisema.
Rais alisema gharama za upigaji simu zimepungua kwa asilimia 57 na huduma za intaneti zimepungua kwa asilimia 75.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi, alisema gharama za upigaji simu zimepungua kwa asilimia 99 na kwamba zimechangiwa na kuwepo kwa mkongo wa taifa wa mawasiliano.
“Ni jambo la kujivunia kuona Tanzania inafanya vizuri kwenye sekta ya mawasiliano kwa Afrika ni ya tatu,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, alisema watumiaji wa simu wameongezeka kutoka milioni tatu mwaka 2005 hadi milioni 27 mwaka jana.
Alisema mtambo huo una faida kuu tano ikiwemo ya kufahamu mapato yatokanayo na simu za kimataifa, kuzuia matumizi ya simu bila ya leseni na kudhibiti matumizi ya simu zisizo halali.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma, alisema sekta ya mawasiliano nchini inaendelea kukua kwa haraka na kwamba hivi sasa kuna laini za simu milioni 28, vituo vya radio 84 na televisheni 27.
Alisema mtambo huo unauwezo wa kuzuia matumizi ya simu kwa kampuni zisizo na leseni.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TCRA, Mhandisi Salmin Salmin, alisema mtambo huo unaboreshwa na kuendeleza huduma za watumiaji.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru