Wednesday 12 February 2014

Wabunge waonywa kutokuwa wabinafsi.

Na Hamis Shimye

MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amewataka wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba kuijadili rasimu ya katiba kwa misingi ya Utanzania na si matakwa binafsi.
Amesema mchakato huo ni mgumu, hususan kutokana na kushirikisha binadamu ambao wana mtazamo tofauti lakini kinachotakiwa ni maridhiano na ikishindikana sanduku la kura liachwe liamue.
Dk. Bilal amesema wanasiasa wanapaswa kuweka kipaumbele katika kukubaliana kwa hoja na kwamba, viongozi wa vyama vya siasa wana wajibu mkubwa katika kusimamia hilo.
Makamu wa rais alisema hayo jana katika kongamano la siku mbili lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa, wakiwemo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, mawaziri na viongozi wa vyama vya siasa nchini.
“Tukikubaliana na kupata maridhiano tutaweza kupata katiba ya Watanzania, itakayoendeleza misingi ya kuvumiliana na amani, kwa kuwa katiba ni suala muhimu,’’ alisema.
Alisema kumekuwapo kauli mbalimbali, hususan katika suala la Muungano, ambapo ofisi yake inayojishughulisha na mambo ya Muungano inaona kuna umuhimu mkubwa wa kubaki kama ulivyo.
“Muungano bado una umuhimu mkubwa na ningependekeza kuna mambo kama mawili ambayo yangewekwa katika Muungano, ikiwemo afya na elimu, kwa kuwa masuala haya ni muhimu,’’ alisema.
Dk. Bilal alisema lazima wajumbe wahakikishe zinatolewa hoja za kuuboresha Muungano na si kuuvunja.
“Hakuna binadamu anayejua zaidi ya mwingine, serikali tunakwazwa na kauli za vitisho. Vyama vya siasa vinapaswa kuonyesha mfano kwa wengine,’’ alisema.
Makamu wa rais alisema anatambua vyama vimeanza kuingia katika joto la uchaguzi lakini visikubali likaharibu mchakato mzima wa katiba mpya.
Alisema katiba ni ya Watanzania na si ya vyama vya siasa, hivyo hakuna haja ya kuzungumza kwa jazba au kutoana ngeu, bali wasimame pamoja katika kupata katiba.
Awali, Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia, alisema katiba ni suala muhimu na lazima maridhiano yawepo katika upatikanaji wake, ili kizazi kijacho kiweze kufaidi matunda.
“Tumekutana ili kuonyesha umoja wa taifa letu na tunapongeza juhudi za serikali katika suala hili. Katiba tunayoitaka iwe ya maridhiano, iliyowashirikisha Watanzania wote,’’ alisema.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema kongamano limepewa kaulimbiu ya tafakuri na maridhiano kuelekea katiba mpya na wanasiasa wanapaswa kuwa wamoja katika kujadili suala hilo.
Alisema anaamini zipo changamoto katika suala hilo lakini watakaa pamoja na watavuka salama kwa kuwa kinachohitajika ni busara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisema katiba ni suala muhimu na katika mchakato wa maoni wananchi walitoa maoni mbalimbali ili yawemo katika katiba.
Alisema suala la Muungano lilijadiliwa kwa kina na lina umuhimu mkubwa kwa kuwa likiachwa litaibua mgogoro wa kikatiba kwa wananchi kuhusiana na mambo mbalimbali.
“Hata ndani ya tume kulikuwepo mawazo na kuna mgawanyiko hasa kutokana na wapo wanaoamini katika Muungano wa serikali moja, mbili na tatu huku wengine mkataba. Tumeanza na serikali tatu,’’ alisema Warioba.
Mbunge wa kuteuliwa katika Bunge Maalumu la Katiba, Profesa Ibrahimu Lipumba, ambaye ni Mwenyekiti wa CUF, alisema uvumilivu unahitajika na kinachotafutwa ni katiba ya Watanzania.
“Tuheshimiane katika maoni kwa kuwa kinachotafutwa ni katiba ya Watanzania na si ya chama fulani, hivyo tuvumiliane katika utoaji maoni,’’ alisema.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema katiba ni suala muhimu hivyo vyama visiingize maoni binafsi katika mambo mbalimbali kwa kuwa wananchi wameshaamua.
Mkutano huo unaendelea leo, ambapo maazimio yatafikiwa, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru