Sunday 16 February 2014

Wabunge kulamba 300,000 kwa siku

Na Mwandishi wetu

KITENDAWILI cha posho za wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba sasa kimeteguliwa, ambapo imeelezwa itakuwa sh. 300,000 kwa siku.
Tayari wabunge wameanza kuwasili tangu Jumamosi na leo watapewa mafunzo maalumu ya namna ya kutumia ukumbi na miundombiu mingine ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema jana kuwa malipo hayo yatahusisha posho ya kikao sh. 80,000 huku posho zingine ikiwemo usafiri, madereva zitakuwa sh. 220,000 kwa siku.
Pia, alisema ukarabati wa jingo pamoja na miundombinu miengine ya ukumbi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wabunge zaidi ya 650, yamegharimu kiasi cha sh. Bilioni 8.2.
Dk. Kashillilah alisema mkutano wa Bunge hilo maalum utazinduliwa rasmi Februari 26, mwaka huu, kesho utafanyika mkutano wa maelekezo ya ukaaji na jiografia ya ukumbi.
Alisema wabunge wameanza kusajili jana na kazi hiyo itaendelea tena leo na kwamba, kesho asubuhi mkutano wa maelekezo utaanza hadi mchana utafanyika uchaguzi wa Mwenyekiti wa muda, kuandaa na kupitisha Kanuni za Bunge.
“Mwenyekiti wa muda atachaguliwa kwa utaratibu maalumu uliowekwa na Katibu wa Bunge la Muungano na wa Baraza la Wawakilishi. Mwenyekiti wa muda atasimamia kuchaguliwa kwa Mwenyekiti na Makamu wake kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Dk Kashillilah.
Alisema Mwenyekiti wa muda pia atasimamia kuandaliwa kwa kanuni na baada ya kupatikana kwa viongozi hao, ndipo Katibu wa Bunge na Naibu wake watateuliwa kwa Sheria.
Pia, alisema kabla ya viongozi hao kuanza kutekeleza majukumu hayo mazito kwa taifa, watendaji hao wataapishwa na Rais Jakaya Kikwete.
Rais Jakaya Kikwete atazindua rasmi Bunge hilo Jumatatu saa 10 jioni na kwamba, wabunge wote wataapishwa siku hiyo saa 4 asubuhi na baadaye kuunda Kamati za Bunge Maalumu.
Uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalumu hilo utafanyika Februari 26 na kwamba, mjadala wa kupitisha Rasimu ya Katiba na utahitimishwa Aprili 30, mwaka huu.
Kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Bunge Maalumu litakuwa na mamlaka ya kujadili na kupitisha masharti ya
Katiba inayopendekezwa na kutunga masharti ya Mpito na masharti yatokanayo kama Bunge Maalumu litakavyoona inafaa.
Ili Katiba inayopendekezwa iweze kupitishwa katika Bunge Maalumu la Katiba, itahitaji kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi
ya wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka Zanzibar.
Bunge Maalumu la Katiba litakuwa na wabunge 629 ikiwa ni wa Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi pamoja na wale wa kuteuliwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru