Sunday 16 February 2014

Kesi ya Wachina wa meno ya tembo leo

NA FURAHA OMARY

KESI ya kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya sh. bilioni 5.4, inayowakabili raia watatu wa China, inatarajiwa kuanza kusikilizwa leo.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Huang Gin (50), Xu Fujie (22) na Chen Jinzhan (31), ambao watapanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Isaya Arufani.
Mbele ya Hakimu Arufani, mashahidi wa upande wa mashitaka wataanza kutoa ushahidi kuhusu mashitaka yanayowakabili Gin na wenzake ambao wanasota rumande.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa baada ya upande wa jamhuri kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali.
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu ya kukutwa na vipande 706 vya meno ya tembo, vyenye uzito wa kilogramu 1,889, vikiwa na thamani ya sh. 5,435,865,000 wakivimiliki bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Katika shitaka la kwanza, wanadaiwa siku na tarehe hiyo, washitakiwa kwa pamoja walikutwa na ganda la risasi lililotumika bila ya kuwa na kibali.
Pia, wanadaiwa siku hiyo walitaka kutoa hongo  ya sh. 30,250,000 kwa maofisa wa polisi, Mrakibu msaidizi wa polisi, Heri Lugaye, Gerwin na ofisa wa wanyamapori Simon Saye na watu wengine waliokuwepo eneo la tukio ili wasiwakamate.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru