Wednesday 19 February 2014

Kingunge awafunda wajumbe bunge la katiba

Na Theodos Mgomba, Dodoma

MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Kingunge Ngombale –Mwiru, amewataka wajumbe wenzake kutanguliza mbele uzalendo wakati wa kupitia Rasimu ya Pili ya Katiba badala ya kuendekeza ubinafsi.
Kwa mujibu wa Kingunge, lengo la bunge hilo ni kupata katiba bora itakayolifikisha taifa katika miaka mingine 50 na si ya chama au mtu fulani. 
Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa bunge baada ya kikao kuahirishwa.
Kwa mujibu wa Kingunge, ni muhimu kwa wajumbe kuthamini nafasi waliyoipata kwa kufanya uamuzi sahihi kuhusu hatima ya nchi na vizazi vijavyo.
Alisema katiba inayoandikwa si ya CCM, CHADEMA au CUF, bali ni ya Watanzania wote.

“Kama wataweka uzalendo mbele bila kujali itikadi za vyama, tutapata katiba bora ambayo itawasaidia wananchi  kwa vizazi vingi vijavyo,” alisema.
Alisema bunge hilo ni chombo kikubwa katika historia ya nchi.

Naye Peter Orwa, mwandishi mwingine aliyeko Dodoma ametaarifu kuwa:

MWENYEKITI wa Muda wa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho, amewateua wajumbe 20 watakaomshauri ili kuleta ufanisi wa utendaji.
Wengi kati ya walioteuliwa ni wataalamu wa sheria, wakiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angelah Kairuki na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA Tundu Lissu.
Wateule hao wanatoka pande zote mbili za Muungano.
Kificho alisema amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa kisheria. Alisema wajumbe hao watakuwa wakifuatilia vikao kwa kuchukua dodoso muhimu za kufanyia kazi na watakutana naye kujadili na kufanya uamuzi.
Wamo pia Profesa Costa Mahalu na Magdalena Rwebangira, ambao juzi waligombea nafasi ya mwenyekiti wa muda wa bunge hilo.
Wengine ni Abubakar Khamis Bakari, Mgeni Hassan Juma, Usi Jecha Simae, Ismail Jusa Ladu, Profesa Abdul Shariff,  Agila Hila Vuai, Dk.Tulia Akson, Amon Mpanju, Elizabeth Minde, Evord Mmanda, George Simbachawene, Nakazaeli Tenga, Peter Mziray, Honoratha Chitanda na Othman Masoud Othman.
Kificho alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Werema, leo atatoa semina kwa wajumbe kuhusu Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba ambayo iliwasilishwa bungeni jana na wajumbe kugawiwa nakala.
Alisema wajumbe watapewa nafasi ya kuzipitia kabla ya kuzipitisha Jumatatu ijayo ili kuwezesha mjadala wa Rasimu ya Katiba kuanza.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru