Tuesday 18 February 2014

Ulinzi waimarishwa Bunge la Katiba,

Na Theodos Mgomba, Dodoma

ULINZI katika mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba umeimarishwa ikiwa ni pamoja na kuongezwa vituo vya ukaguzi.
Katika vituo hivyo, watu wote wanaoingia na kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge wanakaguliwa kwa kutumia mashine maalumu.
Ulinzi katika maeneo ya nje ya ukumbi pia umeimarishwa kwa kuwapo askari wenye silaha na kunafanyika doria ya askari wa kikosi cha farasi.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, jana wakati wa mkutano wa maelekezo ya ukaaji na jiografia ya ukumbi wa bunge, alisema kila mjumbe ataonekana alipo awapo ndani ya ukumbi au nje.
Alisema hilo linatokana na vifaa vya ulinzi vilivyoko katika jengo hilo kuwa vya kisasa zaidi.

“Nawaomba ndugu zangu wajumbe mtambue kuwa ulinzi umeimarishwa, hivyo hata ukiegesha gari nje, jicho letu linaweza kufika huko,” alisema.
Awali, akitoa taarifa, Mratibu wa Ulinzi wa Bunge, Peter Magati, alisema ulinzi umeongezwa, hivyo wajumbe na wengine wote wanaoingia na kutoka ndani ya ukumbi na jengo la bunge watatakiwa kukaguliwa mara mbili.
Magati alisema sababu ya kuongezwa ulinzi ni kutaka kuhakikisha usalama wa wajumbe unakuwa wa kutosha.

“Nawaomba wajumbe mridhie hali hiyo. Tumejipanga vizuri,” alisema na kuwataka wajumbe kuvaa vitambulisho wawapo ndani ya ukumbi na maeneo ya bunge ili kuwaepushia usumbufu.
Kuhusu mavazi, aliwataka kuvaa yenye staha, vinginevyo watarejeshwa wakabadilishe.

Wakati huo huo, Peter Orwa ameripoti kuwa

KATIBU wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, amesema wasaidizi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wenye watoto wachanga watalipwa posho.
Bila kutaja kiwango cha posho hiyo na ni lini itaanza kutolewa, Dk. Kashililah alisema italipwa pia kwa wasaidizi wa wajumbe wenye mahitaji maalumu.
Dk. Kashililah alisema hayo jana asubuhi wakati wa mkutano wa maelekezo ya ukaaji na jiografia ya ukumbi wa bunge.
Alisema kwa kuzingatia haki ya kunyoyesha, kitatengwa chumba maalumu kwa ajili ya wajumbe hao.
Wajumbe hao wanalipwa posho ya kujikimu ya sh. 80,000 na sh. 220,000 ni kwa ajili ya kuhuhudhuria vikao na kuwalipa madereva.
Dk. Kashililah alisema wajumbe wote watapata huduma ya matibabu bure katika zahanati iliyo ndani ya viunga vya ukumbi wa bunge na katika hospitali za serikali na kwa watakaolazimika kutibiwa katika hospitali binafsi watarejeshewa fedha zao.
Kwa wajumbe wanaovuta sigara, wametengewa eneo maalumu katika mgahawa ulio ndani ya viunga vya Bunge.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru