Sunday 16 February 2014

Miradi mikubwa ya barabara kuanza

Na mwandishi wetu

WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, leo atashuhudia utiaji saini mikataba ya ujenzi wa barabara katika mikoa ya Ruvuma na Mtwara. Miradi hiyo itahusisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kati ya Namtumbo na Tunduru, ambayo imegawanywa katika sehemu tatu ambazo ni Namtumbo – Kilimasera (km 68.20), Kilimasera – Matemanga (km 58.70) na Matemanga-Tunduru (km 60.70).
Tayari Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) ambayo inafadhili ujenzi huo kwa pamoja na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), imetoa kibali kwa ujenzi wa sehemu mbili za kuanzia Namtumbo hadi Kilimasera na Matemanga hadi Tunduru. 
Sehemu kati ya Matemanga na Kilimasera itasubiri kibali kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika, ambacho pia kinatarajiwa kutoka hivi karibuni.
Hii ni mara ya pili kwa sehemu hiyo ya barabara kupata makandarasi. Awali kampuni ya Progressive-Higleig Joint Venture kutoka India ndiyo iliyokuwa imeshinda zabuni hiyo mwaka 2010, lakini baadaye ikasimamishwa kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya kimkataba na kuonyesha udhaifu katika utekelezaji wa mradi huo.
Katika hatua nyingine, pia kutasainiwa mkataba wa ujenzi wa sehemu ya barabara inayoanzia Mangaka mkoani Mtwara hadi Nakapanya (km 70.50) katika mkoa wa Ruvuma.
Vile vile utasainiwa mradi mwingine wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kuanzia Nakapanya hadi Tunduru (km 66.50) utakaotekelezwa mkoani Ruvuma.
Kusainiwa kwa miradi hii ni faraja kubwa kwa wakazi wa mkoa wa Ruvuma pamoja na mikoa yote ya kusini kwani, barabara hiyo ni kichocheo kikubwa kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru