Tuesday 18 February 2014

TANESCO yapokea mitambo ya Umeme

SERIKALI imepokea mitambo miwili ya kuzalisha umeme wa megawati 75 kwa ajili ya mradi wa Kinyerezi I ambao unatarajiwa kukamilika  Oktoba, mwaka huu.
Mitambo hiyo kutoka Marekani, ilipokewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, ambaye alikuwa ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba, katika bandari ya Dar es Salaam.
Maswi alisema mradi wa Kinyerezi I utazalisha megawati 150 na kwamba mitambo hiyo ni ya awamu ya kwanza ambayo itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 75.
"Serikali tunatekeleza ahadi tulizozitoa kwa wananchi katika kupunguza ghrama za uzalishaji umeme. Meli hii kubwa ina shehena ya mitambo ya kuzalisha megawati 75 ambayo tutaisimika Februari 28, mwaka huu," alisema.
Alisema mitambo hiyo haitakuwa na athari kwa kuwa ni ya kisasa na awamu ya pili itawasili nchini mwezi ujao. Mitambo hiyo imetengenezwa na kampuni ya General Electric.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Mramba, alisema kuwasili kwa mitambo hiyo ni hatua za msingi za kutatua tatizo la umeme nchini, ambapo tangu uhuru uwekezaji wake ulikuwa duni.
"Katika historia ya nchi tangu Uhuru hatujawahi kuwa na uwekezaji mkubwa kama huu. Mitambo  ya kuzalisha umeme itatatua suala la uzalishaji umeme hivyo bado usafirishaji na usambazaji. Watanzania tuna mipango mingi inayotekelezeka jitihada za leo (jana) ni sehemu ya mipango hiyo," alisema.
Mhandisi Mramba alisema katika eneo la Kinyerezi kuna miradi minne ambayo ni Kinyerezi I, II, III, IV ambayo itapunguza matatizo ya uzalishaji umeme.
Aliwaomba Watanzania kuwa na subira kwa kuwa matatizo ya umeme yatafika mwisho kutokana na miradi mikubwa iliyopo ambayo utekelezaji wake ni wa makini na madhubuti.
Kwa upande wake, Meneja wa Miradi ya Uzalishaji Umeme TANESCO, Mhandisi Simon Jirima, alisema mitambo hiyo itahifadhiwa katika eneo la mradi na baada ya uzalishaji, umeme utaingizwa kwenye gridi ya taifa.
Mhandisi Jirima alisema mradi huo utagharimu dola za Marekani milioni 183 (zaidi ya sh. bilioni 250).

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru