Wednesday 12 February 2014

JK: Marufuku kuuza meno ya tembo nje

NA RABIA BAKARI

RAIS Jakaya Kikwete, amesema Tanzania haitauza nje shehena ya meno ya tembo yaliyokamatwa katika matukio mbalimbali nchini, ambayo yamehifadhiwa.

RAIS Jakaya Kikwete
Amesema yuko tayari kuamuru meno hayo yachomwe moto iwapo hayatakuwa na kazi mbadala lakini siki kuuzwa nje ya nchi.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi, amesema hatatoa kibali cha kuuzwa meno hayo ili kusaidia harakati za kukabiliana na ujangili nchini.
Alisema hayo juzi usiku, alipozindua mabango ya kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika vita dhidi ya ujangili, akiwa njiani kwenda London, Uingereza, ambako leo atahutubia kwenye mkutano maalumu kuhusu kupambana na ujangili wa tembo.
Mkutano huo umeitishwa na mtoto wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles, ambapo viongozi wa mataifa zaidi ya 50 duniani watahudhuria, Rais Kikwete akiwa kiongozi wa kwanza kuhutubia.
Alisema miaka kadhaa iliyopita Tanzania ilifanikiwa kupambana na wimbi la ujangili lakini mambo yameharibika kutokana na kurejea kwa biashara ya meno ya tembo, ambayo vinara wa ununuzi ni mataifa makubwa.
“Tumewahi kukumbwa na majanga makubwa ya ujangili mara mbili, awamu ya kwanza ilikuwa miaka ya 70 hadi 1980. Wakati wa Uhuru tulikuwa na tembo zaidi ya 350,000 lakini walipungua hadi kufikia 50,000,” alisema.
Kutokana na hilo, alisema mwaka 1989 serikali iliingiza jeshi katika Operesheni Uhai na mikakati mbalimbali ya kupambana na ujangili, ambapo mafanikio makubwa yalipatikana.
Alisema hadi mwaka 2009 idadi ya tembo iliongezeka maradufu na kufikia zaidi ya 150,000 lakini sasa imeanza kuwa mbaya kutokana na kushamiri kwa ujangili.
Kuhusu faru, ambao wanakabiliwa na tishio la kutoweka kwa kasi, alisema mwaka 1989 walibaki wawili katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambapo wote walikuwa majike kabla ya kuingia dume kutoka Hifadhi ya Ruaha na kuanza kuzaliana.
“Sasa tuna faru 32 na tumeingia kwenye rekodi ya faru wanaozaliana kwa haraka duniani,” alisema.
Alisema kuendelea kwa ujangili kunatokana na kuwepo soko la meno ya tembo na nyara zingine.
Rais Kikwete alisema jitihada za ndani pekee haziwezi kuwa na mafanikio makubwa, hivyo ni lazima mataifa mengine yahusishwe.
“Nakwenda London kwa mazungumzo ambayo yalianza mwaka jana, yakilenga kufunga masoko ya meno ya tembo na faru. Nitakwenda kuwaambia wazungumze na wenzao kukomesha biashara ya meno ya tembo,” alisema.
Alitaja masoko makubwa ya meno ya tembo kuwa, Thailand, Vietnam na China na kwamba, yakifungwa ujangili utakuwa historia.
Rais Kikwete alisema pia kumeanza kushamiri biashara ya ngozi za simba,  chui na wanyamapori wengine, ambayo inatishia ustawi wa wanyama hao nchini.
Awali, akizungumza kabla ya kuzinduliwa mabango hayo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa, alisema lengo ni kuchochea ushiriki wa Watanzania katika kupambana na ujangili.
MSIGWA AITWA MSALITI
Katika hatua nyingine, mwandishi wetu anaripoti kuwa, Umoja wa Wabunge wa Hifadhi ya Wanyamapori na Mazingira (TPGSNRCU), umemshukia mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msingwa (CHADEMA), ukidai ni msaliti na mnafiki.
Umoja huo umesema kauli zilizotolewa na Msigwa alipozungumza na mwandishi wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, kuwa serikali haifanyi juhudi za kulinda rasilimali hazina ukweli.
Pia umemtaka Msigwa kuwa mzalendo na kuacha kutoa kauli zinazolidhalilisha taifa kwa lengo la kujipatia umaarufu kisiasa kwa mambo yasiyo na chembe ya ukweli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, katika Ofisi Ndogo za Bunge mjini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa TPGSNRCU, Athumani Mfutakamba, alisema serikali imekuwa mstari wa mbele katika kupambana na ujangili.
Mwandishi wa gazeti la Daily Mail, Martin Fletcher, katika chapisho la Februari 8 na 9 mwaka huu, alimshutumu Rais Kikwete, akidai   ameshindwa kutimiza wajibu wake wa kuwalinda tembo na faru.
Gazeti hilo lilimnukuu Msigwa, ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa, serikali haifanyi juhudi za kulinda rasilimali, taarifa ambazo hazina ukweli.
Kwa mujibu wa Mfutakamba, Rais Kikwete yuko mstari wa mbele kupambana na ujangili na aliidhinisha Operesheni Tokomeza Ujangili.
“Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele kupinga biashara hii haramu kwa nguvu zote, kusema haonyeshi juhudi ni kumdhalilisha,” alisema.
Alisema mwandishi wa gazeti hilo, alipaswa kumuuliza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira, James Lembeli, ili kupata ukweli na si Msigwa, ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo.
Mfutakamba alisema umoja huo unafikiria kuiomba serikali imtake mwandishi huyo aombe radhi kwa kuandika taarifa za uongo na udhalilishaji kwa taifa.
Kwa upande wake, Katibu wa umoja huo, Sylvester Mabumba, alisema wataitaka serikali imuamuru mwandishi huyo kuomba radhi kutokana na taarifa hizo.
Alisema kabla mwandishi huyo hajachapisha habari, alitakiwa kumuuliza Lembeli na serikali ili apate ukweli wa mambo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru