Thursday 13 February 2014

Jopo lakwama kusikiliza rufani.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mohammed O. Chande
NA FURAHA OMARY

JOPO la majaji watano wa Mahakama ya Rufani, likiongozwa na Jaji Mkuu Mohammed Chande Othman, limeshindwa kusikiliza rufani ya mfanyabiashara Kibute Otienyeri, anayepinga adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa ubakaji.
Rufani hiyo haikusikilizwa jana kutokana na mkata rufani kutofikishwa mahakamani.

Kutokana na hilo, majaji hao wamemuelekeza msajili wa mahakama kuwasiliana na magereza ili kuhakikisha anafikishwa mahakamani Februari 19, mwaka huu.

Majaji wengine katika jopo hilo ni   Ibrahim Juma, Bethuel Mmila, Kipenka Mussa na Engela Kileo.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Bernard Kongola, ulidai rufani hiyo ilipangwa kusikilizwa jana na wako tayari lakini mshitakiwa hajapelekwa mahakamani.
Wakili Majura Magafu, anayemwakilisha mkata rufani, alidai hajui gereza ambalo Otienyeri yuko, hivyo ikiwezekana mahakama  iwasiliane na magereza ili kujua aliko mshitakiwa.
Jaji Mkuu Chande alisema kwa mujibu wa kumbukumbu, mara ya mwisho alikuwa gerezani mkoani Arusha. 
Magafu aliomba shauri liahirishwe kwa sababu hajui iwapo mkata rufani anataka iendelee kusikilizwa ikiwa hayupo au la.
Jaji mkuu alisema baada ya kushauriana na majaji wenzake na kulingana na shauri lilivyo, wameamua kuahirisha kwa muda hadi Februari 19, mwaka huu, na msajili awasiliane na magereza ili afikishwe mahakamani.
Rufani hiyo ilipangwa kusikilizwa na jopo la majaji watano kutokana na mapendekezo ya jopo la awali la majaji watatu.
Uamuzi ulitolewa na Jaji Mkuu Chande, Jaji Benard Luanda na Jaji Bethuel Mmila, ulipendekeza rufani hiyo isikilizwe mbele ya jopo la majaji watano ili kupata tafsiri sahihi ya vifungu vya sheria vinavyotumika wakati watoto wadogo wanapotoa ushahidi mahakamani.
Katika kutafsiri vifungu hivyo, majaji hao walielekeza rufani za kutiliwa maanani, ikiwemo namba 56/2005 ya Nguza Viking au Babu Seya na mwanawe Johnson ‘Papii Kocha’ wanaotumikia kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi watoto na za Herman Hanjewele na Hamis Shaban.
Katika rufani ya Otienyeri, inadaiwa Agosti 23 mwaka 2008 saa nne asubuhi, katika kijiji cha Manyiri, Arumeru, mkoani Arusha, alimbaka mtoto wa miaka 11.
Kesi hiyo ilikuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ambayo ilimtia hatiani mshitakiwa na kumhukumu kifungo cha maisha jela kutokana na kuridhika na ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa Jamhuri.
Mshitakiwa hakuridhika na uamuzi huo na kukata rufani Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ambapo Jaji Kakusulo Sambo, alikubaliana na hukumu hiyo na kusema anaamini ushahidi uliotolewa na mtoto ni wa kweli.
Otienyeri alikata rufani Mahakama ya Rufani mbele ya jopo la majaji watatu ambao walipendekeza isikilizwe mbele ya jopo la majaji watano.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru