Monday 10 February 2014

Watatu wafa kwenye ajali za Barabarani jijini Dar

NA JUMANNE GUDE

WATU watatu wamekufa jijini Dar es Salaam, katika matukio ya ajali za barabarani likiwemo la Antony Severine na mwenzake ambao walikufa katika ajali ya gari, huko katika barabara ya Mandela.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala Marietha Minangi alisema ajali hiyo ilitokea juzi, saa nne usiku eneo la Buguruni, kiribu na benki ya KCB.
Alisema gari lenye namba za usajili T 858 CDZ aina ya Toyota Opa iliyokuwa inaendeshwa na Domonick Maliki ilipofika eneo hilo ilimshinda na kuacha njia hatimaye kuwagonga watu wawili waliokuwa wanatembea kwa miguu akiwemo Severine (24) ambaye alifariki wakati akipatiwa matibabu.
Marietha alisema mtu mwingine aliyegongwa ambaye hakufahamika jina lake alifariki wakati akipelekwa hospitalini hapo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.


Kamanda wa Polisi (Ilala) Marietha Minangi
Aidha, Marietha alisema maiti ya Severine imehifadhiwa katika hospitali ya Amana na ambaye jina lake halijafahamika maiti yake imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Katika tukio lingine, mkazi wa Magomeni, Khadija Salum (82) amekufa baada ya kugongwa na basi linalotoa huduma ya Usafiri Dar es Salaam (UDA), huko katika barabara ya Morogoro eneo la Magomeni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wKinondoni Camillus Wambura alisema jana, ajali hiyo ilitokea juzi saa 5.49 usiku katika eneo hilo.
Alisema gari hilo lenye namba za usajili T 685 CPA aina ya Eicher, iliyokuwa ikiendeshwa na Boniface Paul ilimgonga Khadija ambaye alikuwa akivuka kutoka upandea kushoto wa barabara kuelekea upande wa kulia.
Wambura alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala, ambapo dereva wa gari hiyo amekamatwa, huku upelelezi ukiwa unaendelea kuhusiana na ajali hiyo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru