Sunday 16 February 2014

Polisi Dom yajipanga kwa Bunge la Katiba

NA MWANDISHI WETU

WAKATI Bunge Maalumu la Katiba likitarajiwa kuanza kesho, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime, amekutana na viongozi wa serikali za mitaa ili kujadili namna na kuimarisha ulinzi na usalama.
Kamanda Misime, alikutana na viongozi hao juzi ambapa aliwataka viongozi wa mitaa na kata kushirikiana kuimarisha ulinzi katika maeneo yao ili kuhakikisha tukio hilo la kihistoria linafanyika kwa usalama.
Viongozi hao wakiwemo viongozi wa dini, madiwani, maofisa tarafa walikutaka katika ukumbi wa Polisi Dodoma, ambapo walijadiliana na kusisitiza masuala ya ulinzi na usalama katika kipindi hiki cha tukio la kihistoria cha kupata Katiba mpya.
Kamanda Misime, aliwapongeza wenyeviti wa serikali za mitaa kwa kuvifufua vikundi vya ulinzi shirikishi hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa kupata katiba mpya ili kuweza kuzuia uhalifu hasa wa uvunjaji amani.
Aliwaomba viongozi hao kushirikiana katika kupunguza ajali za usalama barabarani pamoja na kujenga utamaduni wa kusema familia yangu haina uhalifu.
Aliwataka wamiliki wote wenye baa na kumbi za starehe kuzingatia sheria za kufungua na kufunga baa na kumbi hizo kwani zimekuwa ni sehemu ya maficho ya wahalifu.
Bunge Maalumu la Katiba linatarajiwa kuanza leo mjini Dodoma, ambapo wajumbe wameanza kuwasili mjini hapa kwa ajili ya kuanza vikao vya bunge hilo vinavyotarajiwa kufanyika kwa siku 70.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru