Wednesday 12 February 2014

Vigogo CCM kitanzini leo

NA MWANDISHI WETU

KAMATI Ndogo ya Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), leo inaanza kuwahoji wanachama sita, wakiwemo viongozi waandamizi kwa tuhuma za kuanza harakati za urais mwakani  kinyume cha utaratibu.

Nape Nnauye

Wanachama hao wanatuhumiwa kufanya kampeni kabla ya wakati, jambo linalodaiwa limekuwa likiwavuruga wanachama.
Ni kutokana na vitendo hivyo, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM (Bara), John Malecela, aliibuka na kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Malecela pia alikitaka Chama kutoa msimamo kuhusu wanachama hao, akisema wafuasi wengine wa CCM wamekuwa wakishindwa kufahamu msimamo wa Chama.
Kamati hiyo inakutana mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti Philip Mangula, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara). Wahusika wote wameshakabidhiwa barua za kuitwa kuhojiwa.
Wanachama watakaohojiwa ni aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, ambaye ni mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Akizungumza na Uhuru jana, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema baada ya kuwahoji makada hao, kamati itatoa uamuzi kwa mujibu wa utaratibu wa Chama na kamati hiyo.
“Uamuzi utategemea ukubwa wa kosa, kama wataona kuna mtu ana kosa wanaweza kumuonya yakaisha katika kamati kwa namna watakavyoona inafaa.
“Lakini kama kutakuwa na kosa kubwa zaidi, kamati itapeleka kwenye Kamati ya Usalama na Maadili kwa ajili ya kutoa uamuzi,” alisema.
Hatua ya kuwaita na kuwahoji makada hao ni utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na uongozi wa juu wa CCM kwa nyakati tofauti kutokana na kukiukwa utaratibu wa Chama na kuleta mgawanyiko.
Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa CCM, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Rais Jakaya Kikwete, alisema viongozi wa aina hiyo hawafai kupewa uongozi na kwamba, kamwe hawatafumbiwa macho.
Aliziagiza kamati za Chama zinazohusika na maadili kutimiza wajibu wake kwa kuwahoji watu wanaolalamikiwa kukiuka utaratibu.
Rais Kikwete alisema baadhi ya makada wamekuwa wakigawa fedha kwenye maeneo mbalimbali na kuwataka wananchi kuhoji wema wa aina hiyo ulioanza kushika kasi hivi karibuni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru