Thursday 20 February 2014

Pandu, Kamati ya ushauri wakutana

Na Theodos Mgomba, Dodoma

KAMATI iliyoundwa kumshauri Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho, inakutana leo kupitia Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu, iliyowasilishwa bungeni jana.
Kificho alisema hayo jana bungeni mjini hapa, alipoahirisha kikao.
Alisema kazi hiyo itafanyika hadi  Jumapili wiki hii.
Mwenyekiti huyo alisema atajiunga na kamati hiyo ili kuangalia ilipofikia katika utendaji na kwamba, itafanya kazi pamoja na makatibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dk. Thomas Kashililah na wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad.
Kificho alisema lengo la kukutana na kamati hiyo ni kupitia vifungu vya kanuni na kuangalia kama kuna jambo la kuongeza au la.
Alisema Jumatatu kabla ya kuanza  majadiliano kuhusu rasimu ya kanuni hizo, kamati itatoa taarifa kwa wajumbe kuhusu kazi iliyofanyika.

“Kamati itaanza kazi kesho (leo) saa tatu asubuhi, itafanya kazi hadi Jumapili nami nitaungana nao kuona walichofanya.
“Jumatatu kabla ya kuanza majadiliano, mjumbe mmoja wa kamati au wawili watapewa nafasi ya kutuambia nini kimefanyika, na nini kimeongezwa ili tuwe katika njia sahihi wakati tunajadili,’’ alisema.
Mwenyekiti Kificho aliwaasa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuwa waungwana wakati wa kujadili kanuni hizo na pia kuvumiliana wakati mjumbe akitoa  hoja.
Alisema majadiliano yatakayoanza Jumatatu ni mwanzo wa kuelekea katika majadiliano ya kina kuhusu Rasimu ya Katiba.

“Watanzania wanasubiri tuwasaidie kufanya kazi hii, hivyo ili tuweze kuwatendea haki ni muhimu kufanya kazi kwa weledi na urafiki mkubwa,’’ alisema. 
Kificho, juzi aliwateua wajumbe 20 watakaomshauri ili kuleta ufanisi wa utendaji.
Wengi kati ya walioteuliwa ni wataalamu wa sheria, wakiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA Tundu Lissu.
Pia wamo Profesa Costa Mahalu na Magdalena Rwebangira, ambao Jumanne wiki hii waligombea nafasi ya mwenyekiti wa muda wa bunge hilo.
Wengine ni Abubakar Khamis Bakari, Mgeni Hassan Juma, Usi Jecha Simae, Ismail Jusa Ladu, Profesa Abdul Shariff, Agila Hila Vuai, Dk. Tulia Ackson, Amon Mpanju, Elizabeth Minde, Evord Mmanda, George Simbachawene, Nakazaeli Tenga, Peter Mziray, Honoratha Chitanda na Othman Masoud Othman.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru