Sunday 16 February 2014

JK azionya jumuia CCM

Na Mwandishi wetu

KWA mara nyingine tena, Rais Jakaya Kikwete amezionya jumuia za Chama Cha Mapinduzi (CCM), kujikita katika kuimarisha chama na kujenga mshikamano badala ya kuwa wapigadebe wa makada wanaosaka uongozi.
Amesema jumuia za Chama ni taasisi muhimu na kazi yake kubwa ni kuimarisha na kujenga umoja hivyo, zinapoanza kutumiwa kwa malengo tofauti zinaweza kuleta madhara makubwa na kuzusha mpasuko.
Rais kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, aliyasema hayo juzi wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM mjini Dodoma, ambapo aliwaonya viongozi wote wa jumuia hizo kuacha tabia hizo haraka.
Jumuia ambazo ziko chini ya CCM ina Umoja wa Wazazi, Umoja wa Vijana (UVCCM) na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Kauli ya Rais Kikwete inakuja wakati Chama kikianza kuchukua hatua dhidi ya makada wake wanaotuhumiwa kuvuruga na kukiuka taratibu kwa kuanza kufanya kampeni za kusaka urais katika uchaguzi wa 2015 kabla ya muda mwafaka kufika.
Kutokana na hatua hiyo, Rais Kikwete kwa nyakati tofauti aliagiza kamati zinazohusika na nidhamu kuchukua hatua dhidi ya wanaotaka kukivuraga Chama.
Alisema iwapo jumuia hizo iwe wanachama wake ama viongozi wakianza kujiweka kwenye makundi ya wasaka uongozi, Chama kinaweza kujikuta kwenye mpasuko mkubwa hasa pale wanaowapigia debe wasipopewa ridhaa ya kuwania uongozi.
‘’Kazi kubwa ya jumuia ni kuimarisha Chama na kujenga mshikamano, lakini kuna watu wameanza kuwa wapigadebe wa watu wanaosaka uongozi. Haya mambo hayatakiwi na hatupaswi kuyapa nafasi.

"Mambo yanaweza kuwa magumu pale wagombea mnawaopigia debe watakapokosa nafasi ya kuteuliwa kuwania uongozi. Rudini kwenye kazi mliyopewa na mtambue kuwa hizi jumuia ni taasisi nyeti,’’ alisema Rais Kikwete huku akionyesha kuchukizwa na namna mambo yanavyoendelea.
Juzi, wakati akifungua kikao hicho, Rais Kikwete aliwataka wanachama wa CCM kuacha kuwa wanyonge dhidi ya hila za wapinzania.
Alisema kwa muda mrefu wana-CCM wamekuwa wanyonge na sasa wanapaswa kuwa ngangari pindi wanapofanyiwa vitendo visivyo vya kistaarabu ikiwemo kuumizwa na wafuasi wa CHADEMA.
Mbali na kuimarisha Chama, jumuia hizo ikiwemo UVCCM ndizo zimekuwa na jukumu la kuhakikisha shughuli za Chama zinafanyika kwa amani na utulivu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru