Sunday 16 February 2014

Ndungulile awafunda vijana

Na Emmanuel Shilatu

MBUNGE wa Jimbo la Kigamboni (CCM), Faustin Ndugulile, amewataka vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya.
Ndugulile, alitoa wito huo jana alipokuwa akifungua baraza la vijana la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), Temeke, Dar es Salaam.
Alisema matumizi ya dawa za kulevya yana madhara kwa jamii na taifa na kwamba yanachangia maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Ndugulile, alisema pamoja na juhudi za serikali za kupunguza matumizi ya dawa za kulevya, lakini idadi ya vijana wanaotumia dawa hizo inazidi kuongezeka na kusababisha madhara mbalimbali.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, kati ya vijana wa kike watatu wanaotumia dawa za kulevya, wawili kati yao wameathirika na virusi vya ukimwi na wanaume wawili wanaotumia dawa za kulevya, mmoja ana maambukizi ya ukimwi.
Alisema wakati umefika sasa, vijana kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Ndungulile, ambaye ni mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Temeke, aliwataka vijana kuchagua viongozi wenye sifa watakaowahudumia wananchi.
Katika baraza hilo, Arnord Sangawe, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa jimbo la Temeke na Juma Ndwangila, alichaguliwa kuwa katibu wa jimbo hilo.
Pia, wajumbe wa baraza la UVCCM, walimchagua Yasin Kanyama kuwa mwenyekiti wa jimbo la Kigamboni na Mustafa Pilla, alichaguliwa kuwa katibu wa jimbo hilo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru