Wednesday 12 February 2014

Serikali yafunga mjadala juu ya mashine za EFD

NA MOHAMMED ISSA

SERIKALI imeonya kuwa, mashine za kielektroniki (EFD) zisiwe chanzo cha kuvuruga amani ya nchi, na zitaendelea kutumika kwa mujibu wa sheria.
Imesema msimamo wake uko pale pale na kamwe hautabadilika.
Kwa mujibu wa serikali, hakuna sababu ya kuendelezwa mjadala huo, kikubwa ni wafanyabiashara kufuata sheria za nchi.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, akizungumza kwa simu jana, alisema msimamo wa serikali ni kwamba mashine zitaendelea kutumika.
Alisema wataendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi ya mashine hizo na kwamba, elimu imeshatolewa kwa wafanyabiashara wengi.

“Mashine hizi zipo kisheria, zitaendelea kutumika na tunaomba zisiwe sababu ya kuleta mtafaruku, kuvuruga nchi na kuhatarisha amani,” alisema.
Saada alisema kabla ya kuanza matumizi ya mashine hizo, elimu ilitolewa kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wake na inaendelea kutolewa, hivyo wanaozipinga ni kwa utashi wao.
Waziri alisema madai mengi ya wafanyabiashara kuhusu matumizi ya mashine hizo yameshafanyiwa kazi, hivyo kuwataka kuendelea kuzitumia kama sheria ilivyoelekeza.
Kwa mujibu wa Saada, baadhi ya watu waache wamekuwa wakiwashawishi wafanyabiashara kuhusu matumizi ya mashine hizo.
Kwa takriban siku tatu baadhi ya wafanyabiashara wameingia kwenye mgomo wa kutokufanya biashara wakigomea matumizi ya EFD.
Wafanyabiashara hao, wakiwemo wa maduka eneo la Kariakoo, Dar es Salaam na baadhi ya mikoa, wanapinga matumizi ya mashine hizo, wakiitaka serikali kubadilisha mfumo huo wa ukusanyaji mapato.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru