Thursday 13 February 2014

Wamiliki shule binafsi walia kodi kubwa.

NA TUMAINI MSOWOYA, IRINGA

SHIRIKISHO la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Kiserikali (TAMONGSO) limeiomba serikali kupunguza kodi zisizo za lazima ili kuvutia uwekezaji katika sekta ya elimu.
Kwa kufanya hivyo, TAMONGSO imesema wananchi wa kawaida pia wataweza kumudu gharama za masomo.
Shirikisho hilo limetoa kilio hicho wakati wazazi wengi wakilalamika kuhusu kupanda holela kwa ada za shule binafsi, hivyo kuongeza ugumu wa maisha na kushindwa kuwasomesha watoto.
Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa shirikisho hilo kwa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu, mjini Iringa, Mwenyekiti wa shirikisho hilo,  Celestino Mafuga, alisema wingi wa kodi unasababisha wamiliki kupandisha ada ili kufidia gharama za uendeshaji.
Mafuga alisema kuendelea kupandisha gharama kutawaumiza wananchi wengi, hususan wa kipato cha chini.

“Kodi kubwa kwenye shule zetu inatufanya kupandisha bei ya ada, tutaendelea hivi mpaka lini? Kama nchi inaona elimu ni jambo la muhimu, isaidie kupunguza kodi,” alisema.

Katika hotuba iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Gerald Guninita, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, aliwataka wamiliki wa shule binafsi kupanga viwango vya ada kwa mujibu wa sera ili wasiwaumize wananchi.

Dk. Christine alisema kuwatoza wazazi ada kubwa ni kuwaumiza na ni ukiukwaji wa haki za mtoto katika kupatiwa elimu.
Akitoa mada kuhusu mpango wa uendeshaji shughuli za serikali kwa uwazi (OGP), Ofisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Hadija Maggid, amewataka wamiliki wa shule hizo kuwajibika na kudai mishahara kulingana na utendaji kazi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru