Tuesday, 6 May 2014

Bunge la kufunga mkanda


NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo linaanza kikao chake cha bajeti, huku muda wa kuchangia na kuwasilisha bajeti za wizara ukipunguzwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema, muda wa kuchangia bajeti hiyo umepunguzwa kutoka dakika 10 hadi saba.
Alisema bunge pia limepunguza muda wa uwasilishaji wa bajeti za wizara na kwa sasa kila wizara itapewa siku moja ya kuwasilisha bajeti yake na kujadiliwa.
Kwa mujibu wa Joel, Bunge litaanza kujadili hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu leo jioni.
“Kwa zile wizara ambazo hazina mambo mengi, zitajadiliwa kwa muda wa siku moja na hata muda wa kuchangia tumepunguza na kubaki dakika saba,’’ alisema.
Joel alisema, bunge litaanza kikao chake saa tatu asubuhi kwa kipindi cha maswali na majibu na kisha kupumzika kwa ajili ya kikao cha kupeana ratiba na kisha kurejea saa 10 jioni.
Alisema bunge hilo litaendelea hadi Juni 27, mwaka huu, hivyo wamelazimika kuongeza muda wa kikao hadi kufikia saa nane mchana badala ya saa saba na kisha kuanza tena saa 10 hadi mbili usiku.
“Hatuna muda wa kutosha hivyo hata siku za Jumamosi nazo tutalazimika kuwa na kikao kama kawaida ili kufidia muda,’’ alisema.
Mkurugenzi huyo alisema pia kuwa, wabunge wawili wapya wanatarajiwa kuapishwa leo kabla ya kuanza kwa mkutano wa kawaida.
Aliwataja wabunge hao kuwa ni Ridhiwan Kikwete na Godfrey Mgimwa, ambao walichaguliwa katika uchaguzi ndogo hivi karibuni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru