Tuesday, 6 May 2014

JK: Tutatoa kipaumbele kwa majaji wanawake


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali itateua majaji 20 wa Mahakama Kuu na Mahakama ya  Rufani, ambapo wanawake watapewa kipaumbele zaidi ili kuleta uwiano wa kijinsia.
Pia, amesema serikali ipo katika hatua za ukamilishaji wa mradi wa ujenzi wa Mahakama Kuu katika mikoa minne nchini ili kuendelea kuboresha utoaji huduma kwa wananchi na kuleta haki sawa.
Aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akifungua Mkutano wa 12 wa Kimataifa wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani, ambapo alisema kwa mwaka huu wa fedha, inatarajia kuajiri mahakimu wapya zaidi ya 300 na mwaka 2015- 2016 itaajiri mahakimu wengine 300.
Alitumia fursa hiyo kuwataka washiriki wa mkutano huo kutumia majadiliano hayo katika kuboresha shughuli za kila siku za mahakama ili kutoa haki sawa kwa makundi yote bila ubaguzi.
“Bado kuna changamoto kubwa ya kukosekana kwa haki kwa kuwa sheria nyingi tunazotumia karne hii ya 21 ni zile tulizoachiwa na wakoloni,  kwa sasa zinaonekana kupitwa na wakati,” alisema Rais Kikwete.
Pia, aliwataka watumishi wa mahakama kuacha tabia za upendeleo kwa baadhi ya watuhumiwa wenye uwezo mkubwa kifedha hata kama hawana haki, hali inayonyima wanyonge kupata haki zao.
Rais Kikwete alisema tangu ameingia madarakani, ameongeza idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, ambapo kwa sasa wapo 61 kati yao 27 ni wanawake.
Pia, wapo Majaji wa Mahakama ya Rufaa 19 kati yao wanawake ni wanne.
“Maboresho katika idara ya mahakama hayawezi kufanikiwa bila kushirikisha sekta nzima ya sheria, lazima maboresho hayo yashirkishe idara nzima ndipo tutakapoweza kuwa na sheria nzuri zinaendana na nchi yetu,” alisema
Rais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ), Jaji Mstaafu Eusebia Munuo, alisema mkutano huo ni muhimu utatoa fursa kwa majaji kubadilishana uzoefu utakaosaidia katika utendaji.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande, alisema kwa siku za karibuni watashirikiana na Rais Kikwete kuteua majaji wapya.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru