Tuesday, 6 May 2014

Daladala 1,800 kuondolewa Dar


NA JESSICA KILEO
ZAIDI ya daladala 1,800 hazitaruhusiwa kufanya safari zake maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), kukamilika, imeelezwa.
Pia ujenzi wa miundombinu ya mabasi hayo, unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, ambapo mabasi makubwa 20 na madogo 10 yatatoa huduma za awali kama majaribio.
Meneja Uendeshaji wa DART, Peter Munuo, alisema hayo jana mjini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatua iliyofikiwa hadi sasa.
“Uamuzi huu wa kuondoa mabasi hayo katika miradi yetu utasaidia kupunguza msongamano ambao sio wa lazima maeneo ya mjini yaliyofikiwa na mradi wetu na kukamilika,” alisema na kuongeza kuwa kasi ya utekelezaji hadi sasa ni nzuri.
Akizungumzia kuhusu huduma za majaribio, Munuo alisema itatolewa Desemba, mwaka huu na kwamba huduma kamili zitatolewa Julai, mwakani. 
Meneja huyo alisema Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka, umekwishaanza maandalizi ya kuwezesha kutoa huduma ya awali ya mabasi makubwa kuanzia Kimara Mwisho hadi Kivukoni, ikiwa sehemu ya mafunzo ya mfumo kuanza kutoa huduma.
“Maandalizi ya huduma za awali katika barabara kutoka Kimara Mwisho hadi Kivukoni, ujenzi wa miundombinu, unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu na hivyo tunatarajia kuanza kutoa huduma za awali kwa kutumia mabasi makubwa 20 na madogo 10,”alisema.
“Mabasi haya ya uanzishwaji wa huduma za awali, zitahitajika sh. bilioni 20 kupitia bajeti ya serikali ya mwaka 2014/2015,” alisema Munuo.
Alisema wakati wa huduma hiyo ya mpito, mabasi ya kawaida yataendelea kufanya safari zake kama kawaida na huduma rasmi ya mabasi yaendayo haraka ikianza , zaidi ya daladala 180 zitarudishwa maeneo ya ndani ambako mradi haujafika.
Alisema mabasi ya majaribio yana uwezo wa kubeba abiria  140 hadi 160 mpaka watakapoanza kutoa huduma kamili ifikapo mwakani.
Kwa mujibu wa Munuo, mabasi hayo yatasaidia kupunguza msongamano wa watu unaosababishwa na shida ya usafiri.
Alisema kutokana na tafiti walizofanya ndani na nje ya nchi, mfumo wa mabasi yaendayo kasi  ndiyo unaoweza kupunguza msongamano wa watu na tatizo la usafiri.
Mbali na hilo, alisema wafanyakazi ambao wanafanya kazi katika mabasi hayo watakaokuwa na vigezo, watapata fursa ya kuendelea kufanya kazi kwenye mradi huo.
Kuhusu mradi huo, Munuo alisema umepangwa kutekelezwa awamu sita, ambapo awamu ya kwanza inagharimiwa na fedha kutoka Benki ya Dunia (Dola za Kimarekani milioni 290), huku serikali ikitumia sh. bilioni 23.5 kugharamia ulipaji fidia ya mali zilizoathiriwa na miundombinu ya mradi.
Alisema sekta binafsi inatarajiwa kuchangia Dola za Kimarekani milioni 100 kwa ajili ya kuwekeza kwenye ununuzi wa mabasi na kuanzisha mfumo wa kisasa wa ukusanyaji nauli na utunzaji fedha zinazotokana na mfumo.
Munuo alisema hadi sasa ujenzi wa miundombinu ya awamu hiyo ya kwanza unakwenda vizuri na uko katika hatua mbalimbali na umefikia hatua ya kuridhisha.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru