Tuesday, 6 May 2014

Vuai awaita UKAWA bungeni


Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewakaribisha wajumbe wa UKAWA kujadili na kutafuta muafaka kuhusu katiba mpya.
Akizungumza katika mdahalo wa ‘Tanzania Tunayoitaka’, uliorushwa moja kwa moja na televisheni ya ITV juzi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema lengo la mchakato wa katiba ni kuwa na Tanzania yenye maridhiano.
Akijibu maswali ya washiriki wa mdahalo huo waliouliza kama CCM iko tayari kukaa na UKAWA ili kuzungumza, Vuai alisema imekuwa ni kawaida kwa Chama kukutana na wapinzani, hasa katika kutengeneza maslahi ya taifa.
Alisema CCM ilifanya hivyo katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa Zanzibar, ambapo ilifanikiwa kukubaliana na Chama cha CUF kuanzisha serikali ya umoja wa kitaifa.
Kwa mujibu wa Vuai, ni vyema UKAWA wakarudi na kushiriki kwenye vikao vya Bunge Maalumu la Katiba ili kukamilisha mchakato wa katiba.
“Hata kama UKAWA hawatarudi, wajumbe tulioko tunaendelea na vikao kwa kuwa tunakidhi vigezo vya kisheria vya kutufanya tuendelee.
“Hata hivyo, tungependa warudi tushirikiane kukamilisha mchakato huu kwa maslahi ya taifa,” alisema.
Vuai aliwataka wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kuacha kugeuza mambo, hususan yale waliyoyatumia kutoa mapendekezo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa CUF katika mdahalo huo, ambaye pia ni Waziri wa Afya wa Zanzibar, Juma Duni Haji alimuomba Rais Jakaya Kikwete kukutana na UKAWA ili kuzungumzia mustakbali wao.
Duni alisema iwapo Rais Kikwete hatawaita na kukutana nao, hawatarudi kwenye vikao vya bunge hilo.
Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Hamfrey Polepole, alisema bunge hilo halipaswi kujadili mfumo wa serikali mbili kwa kuwa haliko kwenye raisimu ya mapendekezo ya tume hiyo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru