Tuesday, 6 May 2014

Mvutano mkali Wazazi



  •  Bulembo, Dogo watunishiana misuli
  • Waraka mzito wapenyezwa kwa JK

Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo, amesema ataendelea kufanya kazi za jumuia na Chama na kwamba hatishwi na baadhi ya wanachama wanaopiga kelele.
Pia, amesema jumuia iko imara na itaendelea kuimarika zaidi kutokana na kuvuna wanachama wapya katika ziara mbalimbali alizozifanya nchini licha ya baadhi kumtuhumu kuwa anakwenda kinyume cha taratibu.

Kauli hiyo ya Bulembo imekuja kutokana na madai kutoka kwa baadhi ya wanachama na viongozi wenzake ndani ya jumuia hiyo kuwa anakwenda kinyume.
“Watu wanasubiri kuona Bulembo atasema nini na sisemi ng’o. Wameshafikisha malalamiko kwa Rais Kikwete.
“Wao waendelee kupiga kelele, mimi nachapa kazi. Juzi nilikuwa Mtwara kwenye mkutano wa hadhara, nikarudisha wanachama wengi kutoka upinzani na Mei 15 na 16, nitakuwa na kikao cha Kamati ya Utekelezaji Dodoma kitakachofuatiwa na Baraza Kuu na baada ya hapo nitafanya ziara katika mikoa mitano,” alisema Bulembo.
Bulembo aliitaja mikoa atakayofanya ziara kuwa ni Mtwara, Lindi, Ruvuma, Njombe na Iringa, lengo likiwa ni kukagua uhai wa CCM na jumuia zake na kufanya mikutano ya hadhara.
Kutokana na madai hayo, tayari viongozi hao wamefikisha malalamiko kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, kueleza kasoro hizo na kushusha mzigo wa lawama kuhusu utendaji wa Bulembo tangu alipoteuliwa kushika uongozi.
Habari za kuaminika zinasema kuwa kuna mvutano mkubwa kati ya Bulembo na Makamu wake, Dogo Mabrouk, ambapo baadhi ya makatibu wa wilaya, mikoa na walimu wa sekondari inazozimiliki, wamepanga kuandamana.
Viongozi hao wamepanga kuandamana hadi kwa Rais Kikwete, lengo likiwa kumshinikiza Bulembo ajiuzulu wadhifa huo kutokana na tuhuma mbalimbali zinazomkabili.
Baadhi ya tuhuma dhidi ya Bulembo ni kutumia madaraka yake kuwahamisha mara kwa mara makatibu wa wilaya na mikoa, walimu wa sekondari na kufanya ukarabati wa jengo la ofisi ya makao makuu ya jumuia hiyo bila kushirikisha watendaji wake wakuu, Kamati ya Utekelezaji na mmiliki wa jengo hilo ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). 
Hatua ya makatibu na walimu hao, imekuja siku chache baada ya Dogo kutoa tuhuma nzito dhidi ya Bulembo kutokana na kile anachodai kuwa anatumia vibaya madaraka yake hali iliyomlazimu kumwandikia barua Rais Kikwete, akiweka hadharani tuhuma hizo. 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya makatibu na walimu hao walidai Bulembo amekuwa akitumia madaraka yake kuwanyanyasa kwa kuwahamisha mara kwa mara katika vituo vyao vya kazi bila kuwalipa fedha za uhamisho kama inavyotakiwa kisheria.
Imedaiwa kuwa Bulembo amekuwa na chuki binafsi, hasa kwa makatibu wa wilaya na mikoa, ambao hawakuwa katika kambi yake wakati wa uchaguzi uliomwweka madarakani.
Kuhusu madai ya Bulembo kufanya ukarabati wa jengo la Ofisi za Makao Makuu ya jumuia hiyo, Kariakoo, Dar es Salaam, bila kushirikisha watendaji, imeelezwa kuwa ni moja ya vitendo vya ufisadi vinavyofanywa na mwenyekiti huyo ndani ya jumuia.
Mwaka jana, Bulembo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu, alilazimika kukatisha kwa siku chache ziara hiyo baada ya kuitwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana mkoani Dar es Salaam kujibu malalamiko ya baadhi ya makatibu waliokuwa wamehamishwa vituo vyao vya kazi bila kulipwa haki zao.
Hata hivyo, haikufahamika mara moja kama makatibu hao walilipwa haki zao baada ya kufanyika kwa kikao hicho. Hivi sasa kuna makatibu zaidi ya 45 waliohamishwa katika vituo vyao vya kazi bila kulipwa fedha zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Suzan Omari alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusiana na ukarabati wa jengo hilo, alisema hata yeye anashangaa kama kuna kitu kama hicho kisichofuata sheria.
“Sisi hatujapata barua yoyote kutoka Wazazi ikituomba kufanya ukarabati katika jengo hilo. Kisheria walitakiwa kuleta barua ya maombi ili tuijadili na kutuma wataalam wetu waende kukagua na kujua ni ukarabati wa namna gani na fedha hizo zitalipwa vipi, sasa kama walifanya hivyo ni kosa kisheria,”alisema.
Hata hivyo, alisema kwa sasa yeye (Suzan) yuko likizo, hivyo hawezi kuingia kiundani kuzungumzia suala hilo huku akisisitiza kuwa ni kosa kufanya ukarabati bila kupata baraka kutoka katika shirika hilo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru