Tuesday, 6 May 2014

Mahabusu wazusha tafrani tena kortini


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
TAFRANI kubwa imezuka katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, baada ya mahabusu wa Gereza Kuu la Arusha, kuvua nguo zote hadharani na kubaki kama walivyozaliwa.
Kitendo hicho, kilichotokea jana saa 3:15 asubuhi,  kiliwafanya ndugu wa mahabusu hao na baadhi ya watu waliokuwa mahakamani hapo kukimbia.
Hatua hiyo ya mahabusu kuvua nguo, inadaiwa inatokana na upendeleo wanaopewa  washitakiwa wa dawa za kulevya wenye asili ya Kiasia, ambao walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza April 28 na kesi yao inakwenda haraka tofauti na kesi za washitakiwa wengine.
“Sisi tuna kesi ya kukutwa na dawa za kulevya, hawa wenzetu wanatuhumiwa kwa kosa la kusafirisha dawa, lakini wanafanyiwa upendeleo. Huwa tunakuja mahakamani hapa kila baada ya siku 14, lakini wao wanakaa siku nne tu unawaona wanapelekwa mahakamani.
Kwa nini serikali isitufanyie kama wao,” alihoji mmoja wa mahabusu hao.
Washitakiwa wanaolalamikiwa kwamba wanapendelewa ni Dharam Patel (26) na Nivan Patel (20), wanaodaiwa kusafirisha kete 173 za dawa za kulevya aina ya heroin na  misokoto 300 ya bangi.
Mahabusu hao walifika mahakamini hapo na kuanza kuimba nyimbo mbalilmbali, wakisema wanataka haki zao na baada ya muda mfupi, walianza kuvua nguo zote na kubaki uchi wa mnyama.

Askari magereza waliokuwa ndani ya gari hilo, walimtaka dereva wa basi hilo la magereza lenye namba T 0041 kuliondoa mbele ya jengo la mahakama na kuliegesha mbali kidogo kisha kuanza kuwapiga mahabusu hao.
Hata hivyo, mahabusu hao waligoma kuvaa nguo na kushuka kwenye gari ambapo basi hilo lilirudishwa tena mahali wanaposhukia mahabusu kila siku.
Baada ya kufika eneo hilo, mahabusu hao walilalamika kubanwa na mkojo, hali iliyosababisha mmoja wa askari magereza kutafuta chupa za maji ya Kilimanjaro za ujazo wa lita moja na nusu na kuwapa kisha wakakojoa kwenye chupa hizo baada ya kugoma kukojoa kwenye vyoo vya mahabusu.
Baada ya saa mbili, waandishi wa habari waliomba kibali kwa msajili cha kupiga picha mahabusu hao, lakini askari magereza waligundua na kuliondoa basi hilo mahakamani hapo haraka na kwenda kuliengesha pembeni mwa ofisi za Kamapuni ya Ulinzi ya Foday kwa saa kadhaa.
Akizungumzia kugoma kwa mahabusu hao, Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Willberd Mashauri alisema mgomo huo hauhusu mahakama moja kwa moja kwa kuwa kuna sababu mbalimbali zinazochangia ucheleweshwaji wa kesi zao.
Mashauri alizitaja miongoni mwa sababu hizo kuwa ni baadhi ya vielelezo kama bangi na dawa za kulevya kupelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali ili kuhakikisha kama kweli ni zenyewe.
“Vielelezo vya dawa za kulevya lazima vipelekwe kwa mkemia mkuu wa serikali na kisha vihakikiwe ndipo viletwe mahakamani kwa ajili ya ushahidi,” alisema Mashauri
Kuhusu malalamiko dhidi ya washitakiwa wenye asili ya Kiasia kupendelewa, Mashauri alisema mwendesha mashitaka wa serikali ana mamlaka ya kubadilisha shitaka na wakati mwingine kifungu cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai namba (91)(1), kinampa uwezo mwanasheria mkuu wa serikali kufuta kesi wakati wowote bila  kuhojiwa na mtu yeyote.
Akizungumzia sakata hilo, hakimu aliyekuwa akiendesha kesi hiyo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Mwakuga Gwanta, alithibitisha kwamba kesi hiyo ililetwa mbele yake na ilikuwa imebadilishwa kutoka kusafirisha, ambayo haina dhamana na kuwa ya kukutwa na dawa za kulevya, ambayo inayo dhamana.
“Kesi inayowakabili washitakiwa wanaolalamikiwa iko kwangu na nimeitolea uamuzi wa kuwaachia huru kwa kuwa walibadilishiwa mashitaka ya awali na ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali Arusha ili wafunguliwe mashitaka mapya yaliyoletwa,” alisema.
Hata hivyo, kulionekana kuwepo kwa mkanganyiko mkubwa baina ya Mwamkuga na Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali baada ya mwansheria mmoja wa ngazi za juu katika ofisi hiyo, kukanusha kuwa hajawahi kubadilisha hati ya mashitaka kama inavyodaiwa.
“Hati ya mashitaka iko vile vile, hatujabadilisha, bado wanashitakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya na hawajapewa dhamana kama baadhi ya vyombo vya habari vinavyodai,” alisema.
Washitakiwa hao wawili wenye asili ya Kiasia, watafikishwa mahakamani hapo  Mei 16, mwaka huu kusikiliza kesi inayowakabili kama ina dhamana au la.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru