Tuesday, 6 May 2014


Ghasia anusa rushwa TAMISEMI
Na Latifa Ganzel, Morogoro
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Hawa Ghasia, amesema upangaji wa vituo kwa watumishi wapya ni eneo lenye harufu kali ya rushwa.


Amesema walimu ndio wamekuwa waathirika wakubwa kutokana na watumishi waliopewa jukumu hilo kudai rushwa na kwamba, hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kudhibitiwa.
Amesema hakuna dalili njema kwenye eneo hilo na mianya  ya rushwa iliyopo inatakiwa kuzibwa haraka na kasoro zilizopo zinapaswa kupatiwa ufumbuzi.
Hawa aliyasema hayo juzi wakati akifungua Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu mkoani Morogoro.
Kutokana na harufu hiyo ya rushwa, Hawa alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Jumanne Sagini, kuchukua hatua za haraka kwa watumishi  wote wanaotuhumiwa kwa rushwa au kutoa huduma kwa upendeleo.
Pia alisema mtandao huo ni mpana na unahusisha maofisa kwenye halmashauri, ambao wamekuwa vinara wa kupanga watumishi kwa upendeleo na rushwa.
Alisema wananchi wamekuwa wakipiga kelele juu ya tuhuma za watumishi kupanga vituo kwa upendeleo na kuomba rushwa, hivyo ni wakati wa kuchukua hatua madhubuti.
‘’Ni muda muafaka kukomesha tuhuma hizo kwa kuchukua hatua madhubuti za kuboresha mifumo ya utendaji kazi katika eneo hili,’’ alisema Hawa.
Kwa upande wake, Sagini aliwataka watumishi wa ofisi hiyo kujadili changamoto zinazoikabili ili zipatiwe ufumbuzi wa haraka.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru