Tuesday, 6 May 2014

‘Watendaji wabovu kufukuzwa kazi kwa aibu’


Na Mohammed Issa
SERIKALI imesema itawafukuza kazi kwa aibu watendaji wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), watakoshindwa kutimiza majukumu yao.
Pia imewaonya watendaji wa TBA kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa, vinginevyo watakiona cha moto.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Ibrahimu Iyombe alitoa kauli hiyo juzi mjini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya utiaji saini ujenzi wa makazi ya viongozi na watendaji wa mikoa na wilaya mpya.
Alisema mtendaji yoyote atakayeshindwa kutimiza majukumu yake wakati wa utekelezaji wa mradi huo, atafukuzwa kazi.
Mhandisi Iyombe alisema mradi huo unathamani ya sh. bilioni 18 na kwamba utatekelezwa na TBA.
ìHaitaleta maana TBA waaminiwe na serikali kwa kupewa mradi mkubwa kama huo, halafu wasionyeshe kama wanaweza. Tutahakikisha tunawafukuza kazi watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao,”alisema.
îKatika hili, sitawatetea, sitawaombea wala hatutawafumbia macho, kama mtashindwa kutekeleza majukumu yenu, tutawaondoa,î alisisitiza Iyombe.
Alisema iwapo serikali itaona TBA inashindwa kutekeleza mradi huo, watawanyang’anya na badala yake utatekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Jumanne Sagini aliwataka TBA kutekeleza mradi huo kwa umakini mkubwa.
Alisema ujenzi wa nyumba hizo unajumuisha nyumba za wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wasaidizi wa mikoa na maofisa waandamizi.
Sagini alisema mikoa na wilaya zitakazohusika na ujenzi huo ni Katavi, Geita, Njombe na Simiyu pamoja na wilaya 19 zikiwemo za Kaliua, Uvinza, Kakonko, Gairo, Chemba, Mulele, Kalambo, Wangingíombe, Ikungi, Mkalama, Nyasa, Buhigwe, Momba, Nyanghíwale, Mbogwe, Itilima, Butiama, Kyerwa na Busega.
Alisema mchakato wa kumpata mkandarasi ulizingatiwa kwa kufuata sheria ya manunuzi namba saba ya mwaka 2011, ambapo TBA ilipatikana na kwamba wanatakiwa kujenga majengo 149.
Sagini alisema ujenzi wa majengo hayo utafanyika kwa muda wa wiki 32 na kutaundwa timu kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa mradi huo.
Mwenyekiti wa Bodi wa TBA, Dk. Edward Ngwalle aliwataka watendaji wa wakala huo, kuacha kufanyakazi kwa mazoea na wahakikishe mradi huo unatekelezwa kwa umakini mkubwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru