- Ni Alhad Mussa, aonya asichukiwe kwa itikadi
- Awashangaa wanaomsomea dua bila sababu
- Awapa somo UKAWA, atoa msimamo wa Z’bar
- Balozi Seif: Msajili aichunguze UKAWA kwa makini
NA MWANDISHI WETU
SHEIKH wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, amewataka waislamu nchini kuacha kumshambulia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kwa tofauti za kiitikadi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Sheikh Alhad alisema katika siku za karibuni, kumekuwepo na propaganda zinazowataka waislamu kumchukia Lukuvi bila sababu za msingi.
Alisema hatua hiyo imewafanya baadhi ya waumini kuomba dua maalumu dhidi ya Lukuvi bila kutambua msingi wa hoja hiyo.
Kwa mujibu wa Sheikh Alhad, chuki dhidi ya Lukuvi inadaiwa kutokana na kauli yake ya kupinga serikali tatu kwa kuwa pamoja na mambo mengine, haina vyanzo vya mapato jambo ambalo linaweza kuiweka nchi sehemu mbaya na pengine hata kuchukuliwa na jeshi.
“Tunasema hivyo baada ya kugundua kuwa kuna kundi la fulani la waislamu, ambao ni wafuasi wa chama kimoja cha siasa, ambao wamelibeba suala la hotuba ya Lukuvi kwa mlengo wa kisiasa unaowanufaisha.
“Waislamu tukumbuke kuwa dini yetu inatufundisha kuwa kumchukia mtu kusitufanye kutomtendea haki. Hivyo ni vizuri tukamtendea haki hata kama hatokani na chama chako unachokipenda au si muumini wa dini yako.
“Tunawaomba waislamu kutokubali kutumiwa na vyama vya siasa kwa maslahi binafsi, jambo ambalo linaweza kusababisha chuki miongoni mwetu pasipo na sababu za msingi,” alisema.
Akizungumzia suala la Zanzibar kuwa dola ya kiislamu, alisema Lukuvi aliwasaidia waislamu kujua wasiwasi walionao viongozi wa serikali kuhusu Zanzibar na kwamba huo ndio mlengo wa wanaotaka kujitenga kwa kuachana na Tanzania Bara.
“Mimi sioni dhambi kama Wazanzibar watajitenga na kuwa nje ya muungano na kuanzisha dola ya kiislamu nje ya muungano,” alisema.
Katika hatua nyingine, aliwataka viongozi wa UKAWA kurudi katika meza ya majadiliano pamoja na wenzao wa chama tawala ili kukubaliana na kukamilisha mchakato wa katiba.
Alhad alisema kilichofanywa na UKAWA kutoka kwenye vikao vya Bunge Maalumu la Katiba na kwenda kwenye mikutano ya hadhara, hakutasaidia kupatikana kwa katiba mpya.
Alisema hatua hiyo itachochea vurugu na uvunjifu wa amani ya nchi, jambo ambalo si vizuri kuliacha liendelee.
UKAWA mikononi mwa Msajili
MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, ameombwa kuliangalia kwa umakini kundi la Umoja wa Katiba ya Watanzania (UKAWA), ambalo limeanza kuendesha mikutano ya hadhara inayoashiria mfumo wa kisiasa bila ya kuzingatia taratibu za kisheria.
Ombi hilo limetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Balozi Seif Ali Iddi, wakati akisalimia kwenye mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika katika Uwanja wa Kibanda Maiti Mjini Zanzibar.
Balozi Seif, ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alisema kundi hilo lililoundwa na baadhi ya viongozi wa juu wa vyama vya kisiasa vya upinzani, limeshindwa kutekeleza kazi waliyotumwa na wananchi ya kutengeneza mfumo wa kupata Katiba mpya kupitia Bunge Maalum la Katiba.
Alisema kitendo cha viongozi hao ambacho kinawakosesha wananchi lile wanalolihitaji, kinafaa kiangaliwe kwa umakini na msajili wa vyama vya siasa kwa vile kinaweza kuwakosesha wananchi hao muda wao wa kushughulikia mahitaji yao ya kimaendeleo na kujikita zaidi katika mikutano hiyo yenye ushawishi zaidi wa kisiasa.
Balozi Seif aliwatahadharisha wana- CCM na wananchi wote kujiepusha na kundi hilo ambalo limekuwa likichukuwa kodi zao bila ya kutekeleza majukumu waliyowakabidhi.
“Kama kweli wana uchungu na nyinyi wananchi, mbona walisubiri kwanza kutia mfukoni mkwanja (posho) halafu ndio wakaingia mitini kuvikimbia vikao vya Bunge Maalumu kwa kujenga hoja,“ alisema Balozi Seif.
Aliwaonya wale viongozi wa siasa wenye tabia ya kumsakama katika majukwaa ya kisiasa, kuachana na tabia hiyo mara moja kwa vile wengi kati yao anawaelewa udhaifu wao wa kisiasa.
Alisema iwapo viongozi hao wataendelea na hulka hiyo, waelewe kwamba muda si mrefu atalazimika kufichua maovu na aibu zao.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru