Tuesday, 6 May 2014

Bilal awaasa viongozi wa dini


Na Mohammed Issa
SERIKALI imewataka viongozi wa dini kuwa wavumilivu katika kujenga mshikamano na utulivu nchini.
Pia imeonya kuwa, iwapo amani na utulivu uliodumu kwa miaka mingi vitatoweka, itakuwa vigumu kuvirejesha.
Imesema  makundi ya dini ni muhimu katika kuhamasisha amani ya nchi na kuleta maendeloeo.


Kauli hiyo ilitolewa jana na Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharibu Bilali alipokuwa akifungua kongamano la viongozi wa dini, lililokuwa linajadili amani, demokrasia na maendeleo, lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Dk. Bilal alisema kongamano hilo linawakutanisha pamoja viongozi wa dini mbalimbali na linalenga kujadili amani na maendeleo ya nchi.
Alisema waumini wa dini wanapaswa kudumisha amani na utulivu kwenye jamii zao ili kuziepusha na machafuko yasiyo na lazima.
“Kama amani itatoweka, si rahisi kuirejesha, hivyo tunapaswa kuilinda na kuitunza amani iliyopo kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema.
Kwa upande wake, Msaidizi wa Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubery, aliiomba serikali kuendelea kushirikiana na viongozi wa dini katika kudumisha amani ya nchi na maendeleo ya taifa.
Alisema viongozi wa dini wapo karibu na jamii na kwamba wanaamini hilo ni daraja muhimu la kuleta maendeleo.
Aliongeza kuwa dini isitumike kwa maslahi ya watu na wala isiporwe kwani, inaweza kuiingiza nchi kwenye machafuko.
Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT ), Askofu Dk. Alex Malasusa, alisema kuna umuhimu mkubwa viongozi wa dini, kudumisha amani na utulivu kwenye nchi zao.
Alisema lengo la kongamano hilo ni kuwaweka pamoja viongozi wa dini wa ndani na nje pamoja na wanasiasa katika kuzungumzia umuhimu wa amani na maendeleo duniani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru