Na Abdallah Amiri, Igunga
WALIMU zaidi ya 125 wanaofundisha shule mbalimbali wilayani hapa, wameandama na kufunga ofisi ya mkurugenzi wa manispaa hiyo.
Ofisi hiyo ilifungwa ili kushinikiza walipwe mishahara na posho zao wanazodai kwa kipindi cha miezi minne.
Kufungwa kwa ofisi hiyo kulisababisha wafanyakazi wa halmashauri kukaa nje ya ofisi na huduma kusimama kwa saa tano.
Mmoja wa walimu hao, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema wanasikitishwa na kitendo cha kucheleweshwa mishahara yao na posho zao kwa kuwa ni kitendo cha kinyama.
Alisema tangu wapelekwe wilayani humo, wamekuwa wakifuatilia mishahara na posho bila mafanikio na muda mwingine wakipoteza nauli zao kwenda ofisini hapo.
Hata hivyo, walimu hao walisema wameamua kufunga ofisi ya mkurugenzi ili atambue wanaishi mazingira magumu.
“Sisi walimu tunasikitika sana, mishahara na posho ni haki yetu kwani maisha tunayoishi vijijini ni magumu,’’alisema mwalimu huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa halmashauri, Rustica Turuka alisema mishahara yao bado haijaletwa kutoka hazina, hivyo anawaomba walimu kuvuta subira.
“Nawaomba rudini katika sehemu zenu za kazi, mimi sina lengo baya na nyie kwani hizo fedha ni mali zenu, lakini tatizo liko hazina,”alisema.
Mkurugenzi huyo alisema amejipanga kutafuta sh. milioni 44 ili waweze kuwakopesha walimu hao kwa ajili ya kuwasaidia wakati wakisubiri mishahara yao, ambayo hakuweza kutaja kiwango cha mishahara na posho wanazodai walimu hao.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wilaya ya Igunga, Alphonce Kasanyi alisema walimu hao waendelee kuvuta subira wakati serikali ikishughulikia mishahara yao.
Tuesday, 6 May 2014
Walimu wamfungia DED ofisini
08:32
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru