Saturday 21 December 2013

Bunge lafuta kodi ya simu


Na Theodos Mgomba, Dodoma
BUNGE jana lilipitisha muswada wa marekebisho ya sheria ya ushuru wa bidhaa wa mwaka 2013 kwa kufuta kodi na ushuru wa sh. 1,000 kwa kadi za simu kwa kila mwezi.
Pamoja na kufuta kodi hiyo, serikali imepandisha kiwango cha ushuru wa huduma ya mawasiliano kutoka asilimia 14.5 hadi 17 ili kufidia pengo litakalotokana na kufutwa kwa kodi hiyo.
Akiwasilisha muswada huo kwa hati ya dharura, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema muswada huo umelenga kuanza kutoza ushuru kwa huduma zote za mawasiliano ya kielekroniki.
Alizitaja huduma hizo kuwa ni usambazaji wa mitandao, huduma za kusafirisha taarifa (data), huduma za nukushi na huduma za kusafirisha mawasiliano kwa njia ya waya na zisizotumia za waya.
Alisema kwa upande wa kadi za simu sasa mtumiaji atatozwa kodi kufuatana na matumizi yake.
Muswada huo uliwasilishwa kwa hati ya dharura baada ya Rais Jakaya Kikwete kuweka sahihi urudishwe bungeni kwa ajili ya kufuta kodi ya kadi za simu.
Alisema awali serikali ilitarajia kukusanya sh. bilioni 178 fedha ambazo zilipangwa kutekeleza miradi ya maji na umeme vijijini.
Saada alisema kupandisha kwa ushuru huo wa mawasiliano na kupanua wigo wa kutoza ushuru katika mawasiliano kunatarajia kuipatia serikali mapato ya sh. bilioni 148.
Alisema kampuni za simu zitachangia sh. bilioni 30 ili kukamilisha mapato ya sh. bilioni 178 yaliyolengwa kupatikana wakati wa kukadiria kodi za kadi za simu.
Akizungumzia muswada huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge, alisema imeridhia marekebisho ya muswada huo na kuishauri serikali katika mwaka ujao wa fedha kuangalia uwezekano wa kupunguza asilimia 17 iliyoongezwa katika kodi ya mawasiliano hadi  asilimia 12 ili kuendana na viwango vya nchi za Afrika Mashariki.
Akichangia muswada huo, Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), Mwigulu Nchemba, alisema serikali ilikuwa na nia nzuri ya kuweka kodi hiyo kwa kuamini kutakuwepo na mtambo utakaowezesha watumiaji wa simu kutozwa ushuru kwa kadri wanavyotumia.
Aliiomba serikali kuhakikisha inabana matumizi yake ili Watanzania waridhike kwamba kodi zao zinafanya kazi nzuri ikiwemo kuiona miradi inayotekelezwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru