Wednesday 18 December 2013

Vitalu vya gesi vyatikisa Bunge


Na waandishi wetu
UTOAJI vitalu vya mafuta na gesi nchini umelitikisa Bunge, serikali ikitakiwa kuvitoa kwa kampuni zenye uwezo, ambazo zitakuwa na tija kwa uchumi wa taifa.
Wabunge wameonya vitalu hivyo visitolewe kwa kampuni zisizo na uwezo kwa kigezo cha uzawa, kwani kampuni nyingi za madini zinamilikiwa na Watanzania, lakini hazina mchango au tija kwa maendeleo ya taifa.
Pia wameitaka serikali kuhakikisha inawadhibiti watu wanaopewa vitalu, kwani wapo ambao hugeuka kuwa madalali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, akiwasilisha taarifa bungeni jana, alisema ni lazima mchango wa kampuni zitakazopewa vitalu uonekane na ulete tija kwa Watanzania.
Alisema kampuni za ndani zikiwemo zinazomilikiwa na wazawa kwa asilimia 50 kwa mujibu wa sheria na zilizoingia ubia na kampuni za nje, zipewe upendeleo.
Mwambalaswa alionya kuwa, Bunge lisingependa serikali irudie makosa iliyoyafanya kwenye sekta ya madini kwa kumilikisha vitalu kwa kampuni za watu binafsi, ambao hawataviendeleza.
“Kitendo cha kuwamilikisha watu au kampuni eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 3.886 ambazo ni sawa na asilimia 0.4 ya eneo lote la nchini bila kulifanyia kazi si jambo la busara.
“Mtu anamiliki eneo ambalo ukubwa wake ni mara nne ya mkoa wa Dar es Salaam bila kulifanyia kazi, hili halikubaliki kabisa. Tunataka tuone tija katika hili la vitalu na si ubabaishaji,’’ alisema.
Alisema utaratibu wa wazawa kupata vitalu vya gesi upo wazi chini ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na wazawa hawajazuiwa na hawabaguliwi ilimradi utaratibu wa TPDC ufuatwe.
Mwenyekiti huyo alisema ni vyema wazawa wakaelewa kuwa, uwekezaji katika sekta ya gesi unahitaji fedha nyingi, na wazawa wenye uwezo wanaombwa kujitokeza katika kuwekeza.
“Kamati inawaomba wazawa wenye uwezo kujitokeza na kuacha kulalamika, lakini ikumbukwe kuwa TPDC ni shirika la serikali na umiliki wake ni asilimia 65,’’ alisema.
Alisema ni vyema serikali ikalichukulia suala la kuwa na kampuni ya mafuta ya taifa kuwa la kufa au kupona.
Kuhusu mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, lenye urefu wa kilomita 542, alisema
lina uwezo wa kusafirisha gesi futi za ujazo milioni 784 kwa siku na hadi sasa vipande vya mabomba vyenye urefu wa kilomita 161 vimeunganishwa.
Mwambalaswa alisema ni vyema serikali ikaharakisha utaratibu wa utoaji vibali vya ajira za vijana wa Kitanzania ili waweze kupata uzoefu wakati bomba likikamilika.
Akichangia mjadala huo, mbunge wa Nkasi Kaskazini Ally Keissy (CCM), alimpongeza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kwa jitihada za kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika kwa kutumia gesi asili.
“TPDC ishughulikie masuala yote ya gesi. Gesi inayopatikana popote nchini ni ya nchi nzima na hakuna gesi ya mtu binafsi.
“Nani akubali tukupe kisima wewe na familia yako, gesi ya mtu binafsi anayo tumboni mwake, hatuwezi kumpa mtu na familia yake akamiliki gesi,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru