Wednesday 11 December 2013

Kashfa bungeni


NA ABDALLAH MWERI, Dodoma
WABUNGE wamelipuliwa bungeni kuwa, baadhi yao ni wabadhirifu kutokana na kutumia fedha za umma kinyume cha sheria.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keisy (CCM), aliwalipua wenzake juzi, alipochangia mjadala kuhusu taarifa za kamati za Bunge za Hesabu za Serikali za Mitaa, Bajeti na Hesabu za Serikali Kuu.
Kutokana na hilo, Keisy ametaka sheria ichukue mkondo wake kwa kuwa waliofuja fedha hizo wanafahamika.
Pia ametaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwakagua wabunge wanaotuhumiwa.
Licha ya kukataa kuwataja majina wabunge hao, Keisy alidai ana orodha yao.
Keisy alisema wabunge waliotafuna fedha za walipa kodi watatajwa na CAG, baada ya kuwakagua na kwamba, ikithibitika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria kwa kuwa ni wezi.
“Nashangaa badala ya kuchangia hoja mnaishambulia CCM na serikali, kwani sisi hatujui maovu yenu? Naomba niweke wazi, kuna wabunge wamepewa fedha za safari kwenda kukagua miradi lakini hawakwenda, badala yake walibaki Dar es Salaam.
“Yuko mbunge mmoja mkubwa sana, alikatisha safari akaenda Dubai na mkewe, wako wengine wamepewa sh. milioni tano, sh. milioni sita ili kukagua miradi, badala ya kukaa siku nane wamekaa siku mbili wamerudi Dar es Salaam, kwani hatuwajui?” alihoji.
Kwa mujibu wa Keisy, kigogo mmoja wa chama cha upinzani ana kashfa ya kuingiza kontena la bendera kinyemela, hivyo naye anapaswa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Alisema anashangaa kusikia wabunge wakiwaita mawaziri mizigo, wakati wao ni wabadhirifu wa fedha za serikali.
Mbunge huyo alisema hakuna sababu ya kuwanyooshea vidole mawaziri kwa kuwa wabunge nao ni mizigo kwa wananchi, kwa sababu wameshindwa kusimamia utendaji wao kuanzia katika halmashauri.
Keisy alisema wabunge kwa nafasi zao ni wajumbe wa baraza la madiwani lakini wameshindwa kukemea tabia ya ulaji inayofanywa na baadhi ya watendaji wa halmashauri, badala yake wamekuwa wakiwatwisha msalaba mawaziri.
“Usitake kurusha mawe kwa mpinzani wako wakati unaishi kwenye nyumba ya vioo, hapa ndani mheshimiwa naibu spika kuna wabunge wezi, CAG atawataja baada ya kuwakagua,” alisema.
Baadhi ya wabunge wakichangia mjadala wa taarifa hizo waliishambulia CCM na serikali, wakidai imeshindwa kuchukua hatua dhidi ya watendaji wabovu.
Kabla ya kuahirisha shughuli za Bunge, Naibu Spika Job Ndugai, aliwataka wabunge kutambua kwamba si watendaji wote walioajiriwa serikalini wanatoka CCM.
“Waheshimiwa wabunge nataka kuweka mambo sawa hapa, si watumishi wote wanatoka CCM, lazima tutambue hilo wakati tunachangia mijadala yetu,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru