Wednesday 11 December 2013

Polisi yaua majambazi


Na Nathaniel Limu, Singida
WATU wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi, wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi katika majibizano ya risasi katika kijiji cha Manga nje ya mji wa Singida.
Watu hao ambao walikuwa watatu, wakiwa na bunduki moja ya kijeshi aina ya SMG, walifika kijijini hapo, kwa lengo la kufanya uhalifu kabla ya kupambana na Polisi waliofika kuwadhibiti.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alisema awali walipata taarifa za siri juu ya watu hao na ndipo Polisi walifika kwenye eneo la tukio na kupambana nao.
Alisema watu hao walishtuka baada ya kuhisi wanafuatiliwa na askari polisi, hivyo kuanza kukimbia kuelekea Kjiji cha Uhamaka kwa kutuma pikipiki iliyokuwa na namba za usajili T. 634 BTW aina ya Sanlag.
Hata hivyo, walipoona polisi wanawakaribia, majambazi hayo yaliamua kuitelekeza pikipiki hiyo na kuanza kukimbia porini kwa miguu.
“Yalipoona mambo magumu, yalianza kuwarushia polisi risasi, nao walilazimika kujibu mapigo,” alisema Kamanda huyo.
Alisema katika majibizano hayo, majambazi wawili walijeruhiwa vibaya na baadae kufa wakati wakipelekwa Hospitali ya mkoa Singida kwa matibabu.
Kamwela, alisema majambazi hayo yalijeruhiwa sehemu za usoni, tumboni, shingoni na kifuani na maiti zipo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo.
Aliwataka wakazi mkoani humo wafike hospitali ya mkoa kutambua miili ya watu hao, ambao bado hawajatambuliwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru