Tuesday 24 December 2013

Ongezeko bei ya umeme sawa, lakini...


NA WAANDISHI WETU
WASOMI na wanasiasa wamepokea kwa mtazamo tofauti uamuzi wa kupandishwa gharama za umeme, zitakazoanza kutumika Januari mosi, mwakani.
Wamesema kupanda bei nishati hiyo  kunapaswa kwenda sambamba na utoaji huduma bora ya umeme, na kuimarisha na kuboresha miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA), juzi ilitangaza kupandisha viwango vya bei ya umeme, ambavyo vimepanda kwa kati ya sh. 100 na sh. 306 kwa uniti, kulingana na aina ya watumiaji kuanzia wateja wadogo wa nyumbani, wa kati na wenye viwanda vikubwa. Bei hizo zitadumu hadi mwaka 2016.
Wizara ya Nishati na Madini, imesema imeridhia ongezeko hilo ili kuifanya nishati ya umeme kuwa endelevu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava, alisema jana kuwa, Sera ya Nishati ya mwaka 2003 inaeleza kuwa, gharama za huduma ya umeme ziendane na gharama halisi za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji kwa watumiaji.
Alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa ikitoa ruzuku kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya kuendesha mitambo ya dharura ya kufua umeme, ili kuiwezesha TANESCO kuendelea kutoa huduma.
Mhandisi Mwihava alisema takwimu zinaonyesha gharama za kuzalisha umeme kwa mitambo ya maji ni rahisi, lakini kwa sasa uzalishaji umeshuka kutokana na uhaba wa maji.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mwihava, mitambo hiyo kwa sasa inazalisha megawati 111 wakati uwezo wake ni megawati 561, hivyo kiasi kikubwa cha umeme kinazalishwa kwa mitambo inayoendeshwa kwa mafuta na gesi asilia. Mitambo ya gesi inazalisha megawati 320 na mafuta megawati 210.
Alisema kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu, chenye uwezo wa kuzalisha megawati 204 kwa sasa hakizalishi kabisa kutokana na uhaba wa maji, huku kituo cha Mtera kikizalisha megawati 30, badala ya 80, na Pangani kinazalisha megawati 20 badala ya 68.
Mhandisi Mwihava alisema inapowashwa mitambo ya IPTL na kuendeshwa kwa mwezi mmoja, huigharimu serikali sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya kuzalisha umeme wa dharura ili kuiwezesha TANESCO kuendelea kutoa huduma.
Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa EWURA, Felix Ngamlagosi, alisema juzi kuwa, bei mpya imetolewa baada ya kufanya uchambuzi wa kina wa maombi ya TANESCO.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wasomi na wanasiasa walisema kuna umuhimu wa ongezeko hilo la bei kuangaliwa kwa makini ili liwe na manufaa kwa shirika na wananchi.
Profesa Hosea Kayumbo, alisema si mchumi, lakini kuna umuhimu wa kupandisha bei kwa kuwa itasaidia kuboresha huduma ya umeme na mtumiaji (mwananchi) anapaswa kutekeleza.
“Bei hazirudi nyuma, na suala hili halikwepeki. Wananchi wanapaswa kulipa ingawa kweli ni mzigo mkubwa kwa mwananchi,’’ alisema.
Dk. Benson Bana alisema kupanda kwa bei ni suala nzuri lakini kwa wakati huu si muafaka, kwani ni kuwaumiza wananchi na inaonyesha udhaifu na ukinzani wa sera kati ya serikali na taasisi zake.
“Serikali ipo katika mpango wa kuhakikisha inawaunganishia watu wengi zaidi umeme lakini hapo hapo  mnakuja na tangazo la kupandisha bei. Hii ni kuwaumiza wananchi, hivyo tunapaswa kulitazama kwa makini,’’ alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally, alisema uzalishaji wa umeme uko juu na TANESCO lazima ifidie gharama za uzalishaji. Alisema mwenye jukumu la kuchangia ni mwananchi.
“Tumekuwa tukisikia TANESCO ikizalisha umeme kwa bei kubwa na mauzo yake ni madogo, hivyo lazima itafilisika. Kuongezwa bei kutasaidia kupungua gharama za uzalishaji wa umeme,’’ alisema.
Mwenyekiti wa TLP, Dk. Augustino Mrema, alisema bei hiyo inawaumiza wananchi na kwamba, TANESCO ilipaswa kutatua matatizo yaliyopo na si kupandisha bei ya umeme.
Alisema taifa linakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ya nishati ya umeme, ambao umekuwa wa shida na hakuna uhakika wa upatikanaji wake.
Katika mchanganuo wa viwango vipya vya bei, EWURA imesema wateja wamegawanywa katika makundi matano, la kwanza likiwa D1, ambalo ni la wateja wadogo wa nyumbani wanaotumia uniti 0 hadi 75, ambalo bei imepanda kutoka sh. 60 hadi sh. 100 kwa uniti.
Kundi la pili ni T1, lenye watumiaji wakubwa wa umeme wa nyumbani, wafanyabiashara ndogo ndogo, mashine za kusaga nafaka, taa za barabarani na mabango wanaotumia uniti 76 na kuendelea, ambao watanunua uniti moja kwa sh. 306 badala ya sh. 221 za awali.
Katika eneo hilo, TANESCO walitaka ongezeko la sh. 131 kwa uniti lakini EWURA ilipitisha ongezeko la sh. 85.
EWURA imesema kundi la tatu ni T2 la watumiaji wa umeme wa kawaida, unaopimwa katika msongo wa voti 400, ambao wastani wa matumizi yao kwa mwezi ni zaidi ya sh. 7,500.
Kundi hilo linahusisha  wafanyabiashara wakubwa na viwanda vya kati, ambao watanunua uniti kwa sh. 205 badala ya sh. 132 za awali, sawa na ongezeko la sh. 73. TANESCO iliomba kuongeza sh. 148.
La nne ni kundi la T3- MV, lenye wateja wakubwa waliounganishwa katika msongo wa kati, ambalo EWURA imeridhia  kiwango cha sh. 166 kwa uniti badala ya sh. 121 za awali (ongezeko la sh. 45). Shirika hilo liliomba kuongeza sh. 148 kwa uniti.
Kundi la tano ni la T3-HV la wateja wakubwa waliounganishwa katika msongo wa juu wa voti 66,000 na zaidi, ambao watalipa sh. 159 kwa uniti badala ya sh. 106 za bei ya sasa (ongezeko la sh. 53). TANESCO iliomba kuongeza sh. 80.
Hata hivyo, EWURA imesema bei hizo zitakuwa zikifanyiwa marekebisho kila baada ya miezi mitatu kulingana na mabadiliko ya kiwango cha bei za mafuta, mfumuko wa bei, mabadiliko ya thamani ya fedha na upatikanaji wa ruzuku kutoka serikalini.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru