Wednesday, 11 December 2013

UVCCM yatangaza kiama kwa watendaji


NA SHAABANA MDOE, ARUSHA
MWENYEKITI wa umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Arusha, Martine Munis, amewatangazia kiama watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Ni wale wanaodaiwa kuhujumu juhudi zinazofanywa na Chama na serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Munis alitoa kauli hiyo jana katika ziara ya Kamati ya Siasa ya wilaya ya Arusha, yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika kata za jiji hilo, ikiwemo ya ujenzi, maji, madarasa, nyumba za walimu na utoaji wa mikopo kwa vijana na wanawake.
Akizungumza katika hitimisho la ziara hiyo mjini hapa, alisema haoni sababu ya kupongeza timu nzima ya jiji la Arusha inayo ongozwa na mkurugenzi wake, Sipora Liana, kwakuwa hakuna usimamiza mzuri katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema miradi mingi imetekelezwa chini ya kiwango.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ya vyoo vya wanafunzi katika shule ya msingi Levolosi, vinavyojengwa kupitia mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), vimejengwa chini ya kiwango.
Munis, alisema milango yake imeshaoza na kuanguka muda mfupi kabla ya kukabidhiwa kwa uongozi wa shule hiyo.
Katika shule hiyo, Munis alionyeshwa kukerwa na ujenzi wa nyumba ya walimu ambayo awali mchoro ulionyesha kuwa ni moja kwa mbili na kupewa fedha kwa ajili ya kazi hiyo, lakini kilichofanyika baadaye, nyumba hiyo iligawanywa kwa ukuta na bado haijakamilika ujenzi huku ikihitaji fedha zingine.
Alisema hata tenki kubwa la maji linalojengwa katika Kata ya Sokon One, limeanza kuvuja kabla ya ujenzi wake kukamilika.
Pia, alitolea mfano wa ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Murieti ambao ulitakiwa kukamilika ndani ya wiki sita mpaka sasa haujakamilika japo kwa asilimia 50.
Mhandisi wa jiji la Arusha, Afuilile Lamsi, anataka aongezewe wiki tatu ili akamilishe.
Alisema kuchelewa kukamilika kwa mradi huo wa madarasa kunasababisha kuwakosesha wanafunzi nafasi za kuingia madarasani.
Alisema serikali ilijiwekea malengo kuhakikisha kila mtoto anayepaswa kuingia darasani anaingia.
“Hii itakua ajabu eti wewe una familia ukirudi nyumbani na mkate unataka upigiwe magoti na kusujudiwa, hilo ni jukumu lenu watendaji, hampaswi kukwepa,” alisema.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Dk.Wilfred Soileli, alimtaka Mkurugenzi wa Jiji hilo Sipora na watumishi walio chini yake, kutambua kuwa wameajiriwa na serikali ya CCM, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa Chama.
Hata hivyo, Mkuu wa wilaya ya Arusha, John Mongela, aliagiza dhana ya ushirikishwaji wa kila ngazi husika ya uongozi itekelezwe.
Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi Spora, aliwahakikishia viongozi hao kuwa anatambua kuwa mwajiri wake ni serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, na watumishi walio chini yake wanatambua hilo.
Hivyo watafanya kazi kwa lengo la kutekeleza Ilani ya CCM.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru