Tuesday 3 December 2013

TAMISEMI yahusishwa na ufisadi wa bilioni 2.5/-


 SULEIMAN JONGO NA INNOCENT NGíOKO, MBARALI
OFISI ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeingia kwenye kashfa baada ya baadhi ya watumishi wake kudaiwa kuhusika na ufisadi wa sh. bilioni 2.5 katika Halmashauri ya Wilaya Mbarali, mkoani Mbeya.
Tuhuma hizo zilitolewa jana na Mwenyekiti wa CCM, wilaya ya Mbarali, Mathayo Mwangomo, wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo kilichohudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Mwangomo alisema licha ya hali hiyo, wananchi wamekuwa wakishangazwa na ukimya uliotanda na kutochukuliwa hatua za kisheria kwa waliohusika.
Alisema hatua hiyo inaweza kuwa kikwazo kwa ustawi wa CCM, hasa kuhamasisha imani ya wananchi juu ya Chama.ìKatibu Mkuu moja ya mambo yanayoweza kukiweka Chama katika wakati mgumu ni pamoja na ubadhirifu huo,” alisema.
Alisema licha ya ubadhirifu huo kutambulika hakuna hatua yoyote inayochukuliwa dhidi ya wahusika,  na kusisitiza kwamba umefika wakati kwa Chama kuisimamia serikali.
“Wizara ya TAMISEMI imeoza. Tunafikiri ni muhimu ikasafishwa na
kuwaondoa wote wanaoiharibia sifa nzuri serikali kwa maslahi binafsi,” alisema.
Mara baada ya kusikiliza tuhuma hizo, Kinana alilazimika kumsimamisha mkuu wa mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, ili kutoa ufafanuzi  kuhusu tuhuma hizo.
Kandoro alisema serikali inatambua tuhuma hizo na kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa.
Alisema hivi karibuni alikutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na
kumueleza kuhusu suala hilo, na kuwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na
kukamilika kwa uchunguzi.
Mkuu wa mkoa alisema suala hilo hivi sasa liko katika ofisi ya
Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu, Balozi Ombeni Sefue ambaye tayari
ameshatoa maelekezo kuhusu hatua za kuchukuliwa.
ìUchunguzi umefanyika na ripoti kutoka, ambapo hivi sasa inafanyiwa uchambuzi wa kitaalamu kwa kuwa waliohusika ni pamoja na  watumishi wa TAMISEMI na wa halmashauri ambao baadhi tayari  wameshachukuliwa hatua.
ìBaadhi ya wahusika wametajwa kwa majina. Ofisi ya Katibu Mkuu TAMISEMI, imeandikiwa barua ili kuchukua hatua za kisheria kwa waliohusika,” alisema.
Akizungumzia mgogoro wa mipaka kati ya vijiji vilivyopakana na Pori la Akiba la Mpanga Kipengele na TANAPA, Kandoro alisema hatua  zimeanza kuchukuliwa ili kuweza kumaliza tatizo hilo.
Akijibu hoja na changamoto hizo, Kinana aliitaka serikali kuhakikisha inatafuta ufumbuzi wa kudumu kuhusu mgogoro huo.
Pia, alitaka serikali kutazama upya shamba la Kapunga
lililokodishwa kwa mwekezaji ambaye, hata hivyo, ameshindwa
kuliendeleza.
ìHaiwezekani mwekezaji amekuja kununua shamba lenye ukubwa wa hekta 5,500 halafu anajiongezea hekta 1,830 kinyume cha sheria halafu anaachwa.
ìNafikiri wizara na wahusika wote wanapaswa kulifanyia kazi suala hili haraka ili kuwarudishia wananchi haki ya kumiliki eneo hilo na  kufanya shughuli za uzalishaji,î alisema.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru