Tuesday 10 December 2013

CHADEMA yatakiwa kujipima


NA ABDALLAH MWERI, DODOMA
CHADEMA imetakiwa kujipima kikamilifu kama ina uwezo wa kuleta maendeleo kwa Watanzania, badala ya kukosoa utendaji wa serikali bila sababu za msingi.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Mahmoud Mgimwa (Njombe Kaskazini -CCM), alipochangia taarifa za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Kamati ya Bajeti na Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu.
Mgimwa alisema CHADEMA haina uwezo wa kuwaongoza Watanzania kupata mafanikio, licha ya kuikosoa serikali na CCM kuhusu utendaji wa viongozi wake, wakiwemo mawaziri.
Alisema serikali kupitia CCM imekuwa ikifanya kazi kwa umakini, licha ya kukabiliwa na changamoto za kiutendaji kutoka kwa baadhi ya viongozi walioshindwa kwenda na kasi ya maendeleo.
Mgimwa alisema CHADEMA imekuwa mstari wa mbele kuishambulia serikali lakini imesahau ndani ya chama hicho hawako salama kwa kuwa wameanza kufukuzana.
Hivi karibuni CHADEMA ilimvua madaraka Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
“Tujenge hoja za msingi kwa wananchi na si kushambuliana kwa itikadi za vyama, kwa sababu kama pesa za ruzuku zimeanza kuwaletea shida na mmeanza kufukuzana, je mkipewa nchi mtaweza kweli?” alihoji.
Hata hivyo, ameitaka serikali kupitia mawaziri husika kutoa majibu ya wabunge kuhusu mkanganyiko uliojitokeza katika wizara zao, hususan Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Naye Ally Keisy (Nkasi Kaskazini -CCM), alisema baadhi ya wabunge wamekuwa wakiomba fedha za mafuta ya petroli kwa wakurugenzi wa halmashauri, hivyo nao wanatakiwa kuwajibika na si kuishambulia serikali pekee.
“Wabunge nao wanapaswa kuwajibika, wapo baadhi yetu tunaomba fedha za mafuta kwa wakurugenzi. Tunawajua, kwa msingi huo wote utendaji wetu ni wa kutia shaka,” alisema.
Kwa upande wake, Richard Ndassa (Sumve -CCM), alisema Wilaya ya Kwimba inatarajia kupata huduma bora ya maji, baada ya kuzinduliwa mradi mkubwa hivi karibuni.
Ndassa alikuwa akijibu hoja ya Leticia Nyerere (Viti Maalumu –CHADEMA), aliyedai wilaya hiyo haina mkakati madhubuti wa kupeleka maji na huduma ya elimu.
Mbunge huyo alimtaka Leticia kuhudhuria vikao vya baraza la madiwani, kwa kuwa tayari wilaya hiyo iko katika mpango wa kuzindua mradi mpya wa maji unaotarajiwa kuzinduliwa na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe mwezi ujao.
Ndassa alisema hakuna mwanafunzi katika shule ya wilaya hiyo anayebebeshwa mawe kama alivyodai Leticia.
Moza Abeid (Viti Maalumu -CUF), kwa upande wake ameitaka serikali kutafuta dawa ya mchwa wanaotafuna fedha kupitia mishahara hewa ya watumishi wa umma, kwa kuwa suala hilo limechukua muda mrefu.
Alisema vigogo wa halmashauri wana majibu ya kutambua ufujaji huo wa fedha, kwa kuwa wanafanya kazi kwa karibu na wakaguzi wanaokwenda kukagua fedha za watumishi wa umma, ikiwemo mishahara.
Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini -NCCR Mageuzi), alisema Wizara ya Maliasili na Utalii inatakiwa kusimamia kwa makini watendaji wake, kwa kuwa baadhi ya watumishi ni wala rushwa.
Majadiliano kuhusu taarifa za kamati hizo yanatarajiwa kuhitimishwa leo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru