Wednesday 11 December 2013

Majangili 12,136 yakamatwa


Na Ahmed Makongo, Tarime
BUNDUKI 120, zikiwemo za kivita na majangili 12,136 yamekamatwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika kipindi cha 2003 hadi  mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), ambaye pia ni Mhifadhi Mkuu wa hifadhi ya Serengeti, William Mwakilenga, alisema hayo jana, alipofungua mafunzo ya uandishi wa habari za ujirani mwema.
Mafunzo hayo yanawashirikisha waandishi wa habari, viongozi wa vijiji na wa kimila, na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mwakilenga alisema katika kipindi hicho majangili 15,160 yaliripotiwa kuwepo na 12,136 yalikamatwa, huku zaidi ya 3,000 yakitoroka.
Alisema bunduki 96, zikiwemo za kivita, magobore 30 na risasi 4,375 zilikamatwa.
Katika kipini hicho, mitego ya waya 1,212,584, pinde zaidi 3,000 na silaha nyingine za jadi, ikiwemo mishale zilikamatwa.
Alisema maelfu ya wanyama waliuawa, wakiwemo tembo, huku nyumbu wakiongoza katika idadi ya wanyamapori waliouawa.
Mwakilenga alisema hali hiyo inatisha, kwani ujangili umekuwa ukiongezeka mara kwa mara.
Alisema ni wajibu wa wadau, wakiwemo waandishi wa habari kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa, kwani vikiachwa wanyamapori wote watakwisha, hivyo kuharibu uchumi wa nchi unaotokana na sekta ya utalii.
Kuhusu fidia kwa wananchi ambao mazao yao hushambuliwa na wanyamapori wanaotoka hifadhini, alisema jukumu hilo ni la halmashauri za wilaya kupitia Idara ya Wanyamapori.
Viongozi wa vijiji na kimila waliohudhuria mafunzo hayo, walisema migogoro mingi inatokana na mipaka ya maeneo yao na hifadhi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru