NA MWANDISHI WETU
Wiki inayoanza kesho, ni ya kufanya uamuzi mgumu kwa Rais Jakaya Kikwete kutokana na mtikisiko ulioikumba serikali yake wakati uliopita wa Bunge.
Hivi ndivyo inavyoonekana kutokana na mazingira ambayo yalisababisha mawaziri wane, kujiuzulu na yeye kuridhia kutengua uteuzi wao.
Mawaziri waliojiuzulu na nafasi zao kwenye mabano ni Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la KujengaTaifa), Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi) na Dk. David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi).
Mawaziri hao waling’atuka katika nafasi hizo baada ya ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kubaini matatizo yaliyojitokeza katika Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kutokana na dosari hizo, wabunge waliwataka mawaziri hao kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia watendaji wao wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo.
Mbali na mawaziri hao, wabunge pia walitaka Rais Kikwete amwajibishe Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa madai ya kushindwa kusimamia serikali katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali, ikiwemo kuwepo kwa tuhuma za ubadhirifu uliokithiri ndani Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMESEMI) ambayo iko chini yake.
Wabunge hao walikwenda mbali zaidi kwa kutaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Hawa Ghasia, pia ang’oke na mwenzake wa Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika.
Waziri Hawa alidaiwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya maofisa wa TAMISEMI waliotafuna mabilioni ya fedha wakati Mkuchuka awajibishwe kutokana na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, iliyo chini yake, kuhusika na vitendo viovu wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Licha ya mawaziri hao, Rais ana jukumu la kutafakari na kuchukua hatua dhidi ya mawaziri waliodaiwa kuwa mizigo katika utendaji wao, wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, katika mikoa ya kusini.
Mabadiliko hayo makubwa ya baraza la mawaziri yanatarajiwa kuwa ya tatu tangu Rais Kikwete aingie madarakani mwaka 2005. Mabadiliko ya kwanza yalifanyika mwaka 2008 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, kujiuzulu na mawaziri wengine wawili.
Wengine walikuwa Dk. Ibrahm Msabaha (Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Nazir Karamagi (Nishati na Madini) kutokana na ripoti ya Kamati Teule ya Bunge ilitoundwa kuchunguza mkataba wa ufuaji umeme wa dharura iliyotolewa kwa kampuni ya Richmond Development LLC. Kuwagusa.
Mara ya pili ilikuwa mwaka jana baada ya mawaziri kadhaa kutuhumiwa katika ripoti mbalimbali za kamati za bunge juu ya vitendo vya ubadhirifu na ufisadi.
Mbali na Rais kuwa katika wakati mgumu wa kulisuka upya baraza lake la mawaziri, pia ana kazi ngumu ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, ambalo linatarajiwa kufanyika Februari, mwakani.
Rais katika kutafakuri huko, haishii hapo, kwani pia atakuwa na kazi ngumu ya kufikiria juu ya Ripoti ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na wabunge, kushauri na kutaka watendaji wa serikali, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwajibika kutokana na madudu yaliyojitokeza wakati wa Opereshini Tokomeza Ujangili.
Kutokana na mambo hayo, Rais ataumaliza mwaka na pengine hata kuuanza mwaka kwa kuwa na majukumu mazito ya kufanya.
Wakati Rais akiwa katika wakati huo, pia wapo mawaziri ambao huenda wakamaliza mwaka na wengine kuanza mwaka wakiwa na huzuni ya kutemwa na wengine furaha ya kuteuliwa.
Saturday, 28 December 2013
Wiki ngumu kwa Kikwete
07:40
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru